Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Gerald Mongella, akiambatana na baraza la madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua, Mhe. Jafael Lufungija, Mkurugenzi Mtendaji, ndugu Jerry Daimon Mwaga, pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo, wamefanya ziara ya kujifunza mfumo wa stakabadhi ghalani katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa leo, Desemba 16, 2024.
Ziara hiyo imelenga kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mazao na kuchochea ongezeko la mapato ya ndani kwa Wilaya ya Kaliua na wakulima wake.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Mongella amesema, lengo kuu la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani unaanzishwa na unatekelezwa kwa ufanisi katika Wilaya ya Kaliua ili kuboresha masilahi ya wakulima na kuongeza mapato ya Halmashauri.
“Tumeamua kujifunza mfumo huu ili tufanye vizuri zaidi kwa masilahi ya wakulima wetu na mapato ya Kaliua,” ameisema Mongella.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua, Mhe. Jafael Lufungija, ameshukuru kwa ukarimu wa Halmashauri ya Ruangwa na elimu waliyopata kuhusu mfumo huo.
“Tumejifunza mengi na sasa kilichobaki ni kutekeleza kwa viwango vya juu hata zaidi ya mnavyofanya ninyi,” ameisema Lufungija.
Mbali na hayo. Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa, Nolasco Kilumile, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo, amesisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri na utasaidia kuongeza mapato kwa wakulima na Halmashauri kwa kutoa takwimu sahihi na kudhibiti wizi wa mazao.
Ameongeza kuwa mfumo huo unawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa bei nzuri na fedha kuingia moja kwa moja kwenye akaunti za benki za wakulima.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, amesema kuwa mfumo huo umeimarisha ukusanyaji wa mazao na mapato ya Halmashauri ya Ruangwa, akitoa mfano wa mazao makuu kama mbaazi, ufuta, na korosho.
“Kaliua wakitekeleza mfumo huu, maisha yao yatabadilika kwa kiwango kikubwa,” ameisema Chikongwe.
Hata hivyo, Ziara hiyo pia imewanufaisha wageni hao kwa kutembelea miradi mingine muhimu wilayani Ruangwa, ikiwemo uwanja wa michezo wa Kassim Majaliwa na Shule ya Msingi Likangara iliyojengwa kwa kiwango cha ghorofa.
Ziara hiyo imekuwa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya kiuchumi wilayani, huku ikilenga kukuza mapato ya ndani, maendeleo ya kilimo, na maisha ya wakulima.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa