Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa,Joseph Mkirikiti, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi kusimamia na kuhakikisha Maafisa Misitu wanaandaa mpango kazi na kuwasilisha taarifa ya matumizi ya fedha ambazo wamepokea na kuzifanyia kazi kutoka kwa Mfuko wa Misitu Tanzania( TaFF).
Mheshimiwa Mkirikiti amesema hatua hiyo itaziwezesha Halmashauri kurejeshewa fedha kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za upandaji miti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ruangwa amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bwana Godfrey Zambi alipomuwakilisha kwenye Maadhimisho ya Kampeni ya Upandaji Miti kimkoa yaliyofanyika Machi 15 katika shule ya sekondari Ruangwa wilayani hapo.
Mkuu wa Wilaya Mkirikiti amesema Fedha hizo zinazopaswa kurejeshwa katika Halmashauri ni zinazotoka na wafanyabiashara wa mazao ya misitu ambapo wanapaswa kulipa tozo ya asilimia 5 ya makusanyo kutoka misitu ya asili kwa ajili ya kugharamia shughuli ya upandaji miti Wilayani.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa muongozo huo wa uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, tozo ya asilimia tano ya fedha za upandaji miti inatozwa kwenye mazao ya misitu kama vile kuni, mkaa, magogo, na nguzo.
“Kuna fedha ambazo zinapaswa kurudishwa katika halmashauri zetu kwaajili ya kuratibu shughuli hizi ila watu mnaohusika mnafanya uzembe wa kutokutekeleza majukumu yenu” amesema Mkirikiti
“Wakurugenzi msiwafumbie macho hawa watu wanaotaka kuturudisha nyuma, Kila mtumishi wa serikali azingatie majukumu yake na hakikisheni hizo fedha kwa Halmashauri ambazo hamjazipata watu wenu wawasilishe vitu vinavyotakiwa ili zipatikane” amesema Mkirikiti.
Aidha aliwataka wanafunzi kuwatayari kutunza mazingira yao kwa kupanda miti na kuitunza katika mazingira ya shuleni na hata majumbani kwani wao ndiyo mabalozi wanaotegemewa kuhakikisha mazingira yanakuwa mazuri.
“Miti tunayoipanda leo viongozi ni kwaajili ya taifa la kesho tunawapandia nyie hii miti mjitahidi kuitunza kwani mti inafaida nyingi mtakuwa na vivuli vya kutosha pale mnapohitaji kukaa nje ya madarasa” amesema Mkirikiti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai ,amesema Kilwa ni Wilaya yenye misitu mingi na kuna vijiji vingi vinavyonufaika na misitu hiyo katika kuongeza kipato kwa mtu mmojammoja na Serikali ya kijiji.
Amesema Nanjilinji ni kijiji cha kwanza Kilwa kinachonufaika na utunzaji wa misitu kwani kupitia msitu wake wameishakusanya zaidi ya milioni 800 kwa miaka 5.
“Nanjilinji kupitia misitu wameweza kujenga ofisi nzuri na ya kisasa ya serikali ya kijiji, pia wamejenga nyumba ya kulala wageni na wamejiwekea utaratibu kila mwanafunzi wa darasa la saba anapofaulu kwenda sekondari wanatoa shilingi laki moja kumpa mtoto huyo’’amesemaNgubiagai
Ameongeza kuwa Nanjilinji mwanamke akipata mimba anapewa shilling elfu 50 ya kitanzania kwa ajili ya kusaidia matunzo ya mimba ambapo fedha hiyo inatokana na faida ya misitu waliyoihifadhi kijijini hapo.
Naye Mtendaji wa mradi Usimamizi Shirika rasimali za uvuvi Thomas Chale amesema shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), watashirikiana na viongozi kuhakikisha mazingira ya Mkoa wa Lindi na Wilaya zake yanatunzwa kama inavyopaswa.
Mkoa wa Lindi umefanya maadhimisho ya siku ya upandaji miti kimkoa katika wilaya ya Ruangwa, huku kauli mbiu ikiwa ‘Tanzania ya Kijani Inawezekana Tupande Miti kwa Maendeleo ya Viwanda’.
Mwisho
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa