Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, ameongoza zoezi la kugawa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wadogo leo, Desemba 3, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya, zoezi hilo limekusudia kuwatambua wajasiriamali wadogo wadogo na kurahisisha shughuli zao za kibiashara, huku likilenga pia kuepusha changamoto za ulipaji wa kodi zisizo za lazima.
Akizungumza wakati wa kugawa vitambulisho hivyo, Mhe. Ngoma amesisitiza kuwa vitambulisho hivyo ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo wanaozalisha chini ya shilingi milioni 4 kwa mwaka. Ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwezesha wajasiriamali wadogo wadogo kuendesha biashara zao bila usumbufu, na vitambulisho hivyo vinalipiwa shilingi 20,000 tu kwa miaka mitatu.
“Mhe. Rais ametoa vitambulisho hivi kwa wajasiriamali wadogo wadogo wanaozalisha chini ya milioni 4 kwa mwaka, kama biashara yako inazalisha zaidi ya hapo, waachie wenye biashara ndogo ili nao wapate nafasi ya kujiinua,” amesema Mhe. Ngoma, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia vigezo.
Hata hivyo, kati ya vitambulisho 307 vilivyopokelewa wilayani, ni 15 tu vilivyolipiwa na kugawiwa hadi sasa. Mhe. Ngoma amewahimiza viongozi wa maeneo mbalimbali kuhimiza wajasiriamali wadogo wadogo kulipia na kuchukua vitambulisho hivyo ili kurahisisha uendeshaji wa biashara zao.
“Niwaombe viongozi kuwaelimisha wajasiriamali wadogo wadogo waliopo maeneo yenu juu ya umuhimu wa kulipia vitambulisho na kuvitumia kwa shughuli zao,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya, Ndugu Rashid Namkulala, amebainisha kuwa vitambulisho hivyo vinawahusu wajasiriamali wadogo wadogo kama mama lishe, baba lishe, bodaboda, machinga, na wauza mboga mboga. Hata hivyo, hadi sasa ni wajasiriamali wadogo wadogo 610 waliojisajili kwenye mfumo, kati yao ni 15 tu ndio waliolipia vitambulisho hali inayohitaji juhudi zaidi za kuwafikia walengwa.
Ikumbukwe kuwa vitambulisho hivi vinapaswa kuhuishwa kila baada ya miaka mitatu ili kuhakikisha vinabaki kuwa halali kwa matumizi ya kibiashara. Washiriki wa kikao hicho wameeleza matumaini makubwa ya kuona sekta ya biashara ndogo ndogo ikipata msukumo mpya kupitia mpango huu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa