Timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia wakiongozwa na Mhadhiri Dkt. Joseph Mango, imefanya zoezi la kuweka mtandao mpya wa alama za upimaji na kisha kupima viwanja 90 katika Kijiji cha Mchangani, Kitongoji cha Maguja Wilaya ya Ruangwa, zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Timu hiyo yenye jumla ya watu 8, akiwemo Dkt. Alex Lubida, Dkt. Ijumulana Julian, Mr. Gideon Nchimbi, Ms. Sarah Muneja, Mr. Peter Barongo, Mr. Hassan Kihame na Mr. John Makuri, imeambatana na wanafunzi wa mwaka wa 2&3 wanaofanya mafunzo kwa vitendo (Field) kutoka chuoni hapo.
Kwa Pamoja, wameweka alama kuu saba za upimaji ardhi (control points) katika maeneo ya Mbekenyera Sekondari, Majaliwa Sekondari, Nangumbu “B” (Shule ya Msingi Ng’alile), Shule ya msingi Chingumbwa, Ruangwa/Maguja Sekondari, Mandalawe Sekondari na Liuguru Sekondari. Uwekaji wa alama hizi za msingi za upimaji una faida nyingi kwa Wilaya, ikiwemo kurahisisha upimaji wa viwanja na shughuli nyingine za upimaji.
Kwa upande mwingine, wataalamu hawa wamepima jumla ya viwanja 90 vya matumizi mbalimbali kama makazi na maeneo ya taasisi ikiwemo Ruangwa/Maguja sekondari. Wakati wakiendelea na zoezi la upimaji, walipata pia nafasi ya kuwaonesha wanafunzi vifaa vya upimaji ardhi. Pia walielezea namna vinavyoweza kufanya kazi. Kwa ujumla, yote yalifanywa na wataalamu hawa, yamefanyika kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwa, ikiongozwa na Mkurugenzi ndugu Frank Chonya.
Aidha, Mpima ardhi wa Wilaya ya Ruangwa, ndugu. Raymond Cholobi, amepongeza juhudi za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kusaidia Wilaya ya Ruangwa kwa kuweka mtandao wa alama za upimaji. "Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa msaada mkubwa walionyesha katika kutekeleza zoezi hili. Uwekaji wa mtandao huu ni hatua muhimu ambayo itarahisisha upimaji na matumizi bora ya ardhi katika Wilaya yetu tunathamini sana ushirikiano huu," amesema Cholobi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara huo, Dkt. Joseph Mango, ameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa zoezi hilo lenye manufaa makubwa kwa maendeleo ya jamii ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa