Changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya iliyokuwa inawakabili wakazi wa kijiji cha Mbecha kata ya Nanganga imekuwa historia baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati.
Amesema wakazi hao walikuwa wakipata shida ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji vya jirani mara mtu anapougua ikiwa pamoja na dharura mbalimbali zikiwemo za wajawazito.
Waziri Mkuu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ameweka jiwe hilo la msingi tarehe 01/03/2018, alipowasili mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi katika jimbo la Ruangwa. Ujenzi wa zahanati hiyo umefadhiliwa na Africa Relief Organisation.
“Mbecha mtu akiugua tulikuwa tunapata shida ya sehemu ya kupata huduma ya matibabu, leo matibabu yatakuwa yanapatikana hapa kijijini. Kwa niaba ya wanaruangwa nawashukuru sana viongozi wa African Relief Organisation”Amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu amesema kuwa mkakati wa Rais Dr John Pombe Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya Afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.
“ Jiungeni na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kupunguza gharama za matibabu kwa familia kwani huduma hii mtu anapojiunga ananafasi ya kuwakatia kadi watoto wanne , mke na mume kwa shilingi elf 15,000”amesema Waziri Mkuu.
Awali, Mtendaji wa kijiji cha Mbecha bw. Alfani Ngaeje alisema wazo la ujenzi wa zahanati ya kijiji hiko lilianza mwaka 1987, ambapo utekelezaji wake ulikwama kutokana na hali duni ya kiuchumi iliyokuwa ikiwakabili wakazi wake.
Amesema wananchi wengi wameendelea kupata shida ya kupata huduma za afya hasa kinamama wajawazito na watoto walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye zahanati za vijiji vya jirani.
Hivyo alimshukuru waziri mkuu kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho kwa kuwatafutia mfadhiri aliyewajengea zahanati hiyo ni pamoja na matibabu ya wangonjwa wa nje(OPD),kliniki kwa wajawazito na watoto,chanjo na uzazi wa mpango.
Huduma nyingine ni kuzuia maambukizi wa virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda mtoto,kujifungua,elimu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali. Jumla ya kaya 594 zenye wakazi 2,485 wanatarajiwa kunufaika na zahanati hiyo.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa