Baraza la Michezo la Taifa (BMT) leo tarehe 16 Desemba 2024, limeendesha mafunzo ya michezo kwa walimu wa michezo kutoka shule za msingi na sekondari pamoja na makocha wa vilabu mbalimbali vya michezo katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
Mafunzo hayo yameratibiwa kwa ushirikiano kati ya BMT na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, huku yakitolewa na wataalam kutoka wizara husika ndani ya Baraza pamoja na wataalam wengine kutoka vyama mbalimbali vya michezo.
Aidha, Michezo inayohusika katika mafunzo hayo ni pamoja na mpira wa miguu, riadha, mpira wa kikapu, na mpira wa wavu.
Sambamba na hayo, mafunzo hayo yanatarajiwa kuinua viwango vya ufundishaji michezo kwa walimu na makocha, hatua itakayochochea maendeleo ya vipaji vya michezo mashuleni na ndani ya jamii.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Afisa michezo wa BMT Charles Maguzu amesema lengo ni kuboresha uwezo wa walimu na makocha katika kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi na wachezaji wilayani humo.
“Tunataka kuona michezo inakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla.”
Kwa upande mwingine, Mwl. Sifa Mwaya ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo ameeleza kufurahishwa na fursa hiyo, akisema itasaidia kuboresha mbinu zao za kufundisha na kuendesha michezo kwa weledi zaidi.
“Mafunzo haya ni fursa muhimu sana kwetu, natumini itakuwa hatua muhimu kwa ukuaji wa michezo shuleni na katika jamii.”
Baraza la Michezo la Taifa limeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha maendeleo ya sekta ya michezo yanawafikia wananchi wa ngazi zote.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa