Benki ya CRDB imetoa msaada wa Madawati 20 kwa ajili ya shule ya Msingi Mtopitopi, meza 40 na viti 40 kwa shule ya sekondari Mbekenyera wilayani Ruangwa mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu yake maalumu ya KETI JIFUNZE iliojikita kuwawezesha wanafunzi kupata nafasi ya kujifunza mashuleni wakiwa wameketi.
Hafla hiyo imefanyika mapema Tarehe 10 Julai 2023 katika viwanja vya shule ya msingi Mtopitopi ambapo vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na uongozi wa CRDB Benki kutoka Makao makuu na kanda wakiongozana na meneja wa tawi la Ruangwa.
Suzan Shuma ambae ni Menenja Mwandamizi wa Benki ya CRDB anaesimamia idara ya serikali za mitaa kutoka makako makuu ya Benki hiyo alisema malengo ya kusaidia Viti, Meza na Madawati mashuleni ni sehemu ya programu ya KETI JIFUNZE ilioanzishwa na Benki hiyo kwa malengo ya kuunga juhudi za serikali kama wadau wa maendeleo kupitia sekta ya Elimu na kubainisha kuwa mpango huo unategemewa kufika katika kila wilaya nchini kote ambapo jumla ya madawati meza na viti vipatavyo 5,000 (Elfu tano) vinategemewa kugawiwa na Banki hiyo.
“Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua akijenga Mashule, anatoa elimu bure lakini amekua akitoa madawati katika shule za msingi na sekondari, nasi Benki ya CRDB tunachukua kama sehemu ya kurudisha faida kwa jamii na ndio maana tumekuja na hii program ya keti jifunze kuinga mkono Serikali” alisema Suzan.
Akipokea Meza, Viti na Madawati hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Ndg,Frank Chonya Pamoja na kuishukuru na kuipongeza Benki hiyo ya CRDB kwa kusaidia vifaa hivyo akatumia wasaa huo kuwataka Walimu kuwa waangalizi na wanafunzi wanaotumia vifaa hivyo kuhakikisha wanatunza ili viweze kuwasaidia na vizazi vijavyo.
“Leo serikali ilitakiwa kutoa ela nyingi sana za madawati haya meza na viti lakini tutakwenda kusaidia shule nyingine kwa maana huku wenzetu CRDB wameshatusaidia halafu ndani ya siku mbili muharibu hakikisheni Watoto hamchezi kwenye meza” aliongeza kwa kusisitiza Chonya.
Katika hatua hiyo mkurugenzi Chonya akatumia wasaa huo kuwaeleza wazazi ,walezi na wanafunzi waliofika katika hafla hiyo ya kupokea viti meza na madawati, kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuleta miradi mingi ya kuboresha miundombinu ya Elimu na kwamba hali hiyo hutokana na juhudi za Mbunge wa jimbo la Ruangwa ambae ni Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa anaepaza Sauti kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili wanaruangwa wapate maedeleo.
Baadhi ya wanafunzi walimu na wazazi walioshuhudia afya hiyo wakiwamo Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mtopi Mwl Norbet Machinga, amaeshukuru kupata msaada wa madawati hayo na kusema sasa tatizo la Watoto waliokuwa wakiketi kwa kubanana na wengine kukosa madawati ya kukalia litapungua.
“Tulikua na upungufu wa madawati 78 na kwa msaada huu wa CRDB wa madawati 20 umetusaidia sana Watoto kupungua kukaa chini sasa tutabakiwa na upungufu wa madawati 58, tunawaomba na wadau wengine wajitokeze kutusaidia hayo yaliobaki ili Watoto wetu wapate kukaa kwenye madawati”. Alisema machinga ambae ni mwalimu mkuu shule ya msingi mtopitopi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa