Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa wamepewa mafunzo ya Mfumo wa Inspection and Financial Tracking Management Information System (IFTMIS), leo Jumanne, tarehe 29 Aprili 2025, mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji katika matumizi sahihi ya mfumo wa IFTMIS, ambao ni mfumo wa kidijitali unaotumika katika usimamizi wa taarifa za kifedha na ufuatiliaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma, kupitia mfumo huo majibu ya hoja huandaliwa, kuwasilishwa na kushughulikiwa kwa njia ya kielektroniki.
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Jitetee Mbonde, ameongoza mafunzo hayo akishirikiana na Mhasibu wa Wilaya, CPA Goodluck Swai. Kwa pamoja wameeleza kwa kina jinsi mfumo wa IFTMIS unavyofanya kazi na namna ya kuutumia kwa ufanisi ili kuhakikisha hoja za CAG zinajibiwa kwa usahihi na kwa wakati.
Vilevile, washiriki wa mafunzo hayo wamepata nafasi ya kujadiliana na kuuliza maswali kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza katika matumizi ya mfumo huo. Mafunzo haya yamewasaidia kuelewa vizuri wajibu wao katika mnyororo wa uwajibikaji wa kifedha.
Hata hivyo, viongozi hao wamepongeza jitihada za Halmashauri katika kuwawezesha kiufundi na kuahidi kutumia kikamilifu maarifa waliyopewa ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wao wa kila siku.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa