Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii 151 wa Wilaya ya Ruangwa wamesaini mikataba ya makubaliano ya utendaji kazi na Halmashauri leo tarehe 01 Septemba 2025, ikiwa ni hatua rasmi ya kuanza majukumu yao ya kazi.
Zoezi hilo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na kuongozwa na Mwanasheria wa Halmashauri, Adv. Levina Mlelwa. Tukio hilo limeshuhudiwa pia na viongozi wa Idara ya afya, likiwa ni hatua muhimu ya kuanzisha rasmi ajira za wahudumu hao waliopatiwa mafunzo maalum ya huduma za afya ya jamii.
Aidha, akizungumza katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Feisal Said, amesisitiza kuwa mikataba hiyo ni alama ya kuanza rasmi majukumu ya wahudumu hao, ambapo wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi. Amebainisha kuwa jukumu walilopewa si la kawaida bali ni dhamana kubwa inayohitaji bidii, kujituma na uadilifu katika kuwahudumia wananchi.
“Nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa weledi na uaminifu, kwa sababu wananchi wanatuhitaji na mafanikio yetu yatapimwa kwa utendajikazi eenu.” Amesema Dkt. Feisal.
Zaidi ya hayo, Dkt. Feisal amefafanua kuwa utendaji kazi wa wahudumu hao utapimwa kwa kuzingatia vigezo vya utendaji (key performance indicators), ambavyo ni sehemu ya mfumo wa kitaifa wa upimaji wa huduma za afya. Ameeleza kuwa vigezo hivyo vitawawezesha viongozi kutathmini ubora wa huduma zinazotolewa, ikiwemo ushirikiano na jamii, uwajibikaji na ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Sambamba na hilo, Dkt. Feisal amesisitiza mshikamano na ushirikiano kati ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wataalamu walioko katika vituo vya afya na zahanati. Amesema ushirikiano huo utasaidia kuboresha taarifa za afya, kuongeza kasi ya rufaa kwa wagonjwa na kufanikisha kampeni za kitaifa za afya zinazotekelezwa katika ngazi ya jamii.
Vilevile, amewakumbusha wahudumu hao kufanya kazi kwa weledi na uaminifu, huku wakitekeleza jukumu la kuwafikia wananchi nyumba kwa nyumba. Ameongeza kuwa mtindo huo wa kazi unalenga kuhakikisha kila kaya inafikiwa na huduma za afya.
Kwa upande wao, baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya Jamii waliopata nafasi ya kuzungumza wameonesha furaha na shukrani kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kuwapatia mikataba yao. Wameahidi kuwa tayari kuanza kazi mara moja, kushirikiana na wananchi kwa ukaribu na kuchangia kwa vitendo katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa