Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, leo Septemba 2, 2025, amezindua rasmi zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo katika Kijiji cha Nangumbu, Kata ya Malolo wilayani Ruangwa, zoezi hilo ni hatua muhimu ya kulinda afya ya mifugo na kuinua uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa wakulima na wafugaji wa Wilaya hiyo.
Akisoma taarifa ya uzinduzi huo, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Hassan Mdoembazi, amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepeleka chanjo, vifaa vya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kwa ajili ya kampeni hiyo. Amefafanua kuwa Wilaya ya Ruangwa imepokea chanjo za kuku aina ya tatu chupa 550 ambazo zitatumika kuchanja kuku zaidi ya 110,000 dhidi ya magonjwa hatari yakiwemo kideri, mafua na ndui.
Aidha, chanjo za mbuzi na kondoo ambazo ni chupa 95 zitatumika kuchanja zaidi ya mifugo 9,500 dhidi ugonjwa wa Sotoka, huku chupa 30 za chanjo ya ng’ombe zikitarajiwa kuchanja jumla ya 3,000 dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu.
Akizungumzia umuhimu wa kampeni hiyo, Mdoembazi amesema chanjo na utambuzi wa mifugo vitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao bora ya mifugo, kuimarisha afya za wanyama, kupunguza gharama za matibabu kwa wafugaji na kulinda ustawi wa jamii.
“Hii ni fursa ya kupunguza hasara zinazotokana na vifo vya mifugo na kuongeza kipato cha kaya kupitia mazao bora ya mifugo,” amesema Mdoembazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Ngoma amewataka wafugaji wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kuhakikisha mifugo yao inalindwa na kuwekewa utambulisho sahihi. Aidha, amesisitiza kuwa Serikali imetoa ruzuku kubwa ili kuhakikisha wafugaji wanapata chanjo kwa gharama nafuu huku akiwataka kufanya ufugaji wa kisasa zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi sasa zaidi ya kuku 107,800 wamekwishachanwa, sawa na asilimia 98 ya lengo, huku matarajio yakiwa ni kufanikisha chanjo kwa ng’ombe 3,000 na mbuzi pamoja na kondoo 9,500 katika Wilaya nzima ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa