Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amekagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nambilanje leo tarehe 16 Septemba 2025, ziara hiyo inalenga kufuatilia kasi ya mradi na ubora wa miundombinu inayojengwa.
Katika ukaguzi huo, Mkurugenzi ameambatana na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Feisal Said, ambapo wametembelea maeneo yote ya ujenzi. Mradi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 613 na unajumuisha wodi za wagonjwa wa kulazwa, jengo la wazazi, huduma za wagonjwa wa nje (OPD), kichomea taka, sehemu ya kufulia pamoja na miundombinu ya maji safi na salama, hatua inayolenga kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa viwango bora.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Ndugu Chonya amesema ameridhishwa na kasi ya Mkandarasi na viwango vya ubora vinavyozingatiwa.
“Nimefurahishwa sana na kasi ya Mkandarasi lakini pia ubora umezingatiwa kwa kiwango cha juu, niwaombe tu ujenzi ukamilike mapema ili wananchi wapate huduma bora kwa wakati,” amesema Chonya.
Aidha, Mkurugenzi amebainisha kuwa mradi wa Nambilanje ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na makazi yao. Ameongeza kuwa Serikali inahakikisha kila fedha inayotolewa kwa ajili ya miradi ya afya inatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
Zaidi ya hayo, amewataka wananchi wa Nambilanje na Vijiji vya jirani kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na Mkandarasi. Ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya kituo hicho na kuhakikisha kinawasaidia na kizazi kijacho.
Vilevile, Mkurugenzi amesisitiza kuwa mafanikio ya miradi kama hii yanahitaji mshikamano wa jamii na Serikali. Ameeleza kuwa huduma bora za afya hazipimwi tu kwa majengo mapya, bali pia kwa mshirikiano wa wananchi katika kudumisha usafi, kulinda vifaa na kuunga mkono mpango wa utoaji huduma bora.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Feisal Said, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza changamoto za wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya. Ameeleza kuwa kituo kitakapokamilika kitatoa huduma muhimu za mama na mtoto, chanjo, matibabu ya dharura na magonjwa yasiyoambukiza, hatua ambayo itaongeza usalama wa jamii na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa