Idara ya Mipango na Uratibu ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa leo, Septemba 26, 2025, imeendesha mafunzo maalum kwa Maafisa Bajeti wa Idara/Vitengo kuhusu kuzingatia wakati wa uandaaji wa mipango na bajeti katika Halmashauri, ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, yakiwaleta pamoja Maafisa Bajeti kutoka Idara na Vitengo mbalimbali. Yamelenga kuwawezesha washiriki kuhakikisha kuwa maandalizi, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango na bajeti unafanyika kwa kuzingatia taratibu, miongozo na viwango vya matumizi ya fedha za umma, huku yakiwasilishwa na Maafisa kutoka Idara ya Mipango na Uratibu, wakiongozwa na Pendo Njovu na Upendo Mkangara.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mchumi, Pendo Njovu amesema:
“Mafunzo haya yatawapa ujuzi wa kina maafisa Bajeti katika Idara/Vitengo vyao, wataweza kuandaa mipango na bajeti kwa kuzingatia taratibu, miongozo na uwajibikaji, hivyo tunategemea kuona mabadiliko makubwa zaidi” amesema Njovu.
Aidha, mafunzo yamewapa washiriki mwongozo wa kina kuhusu mbinu bora za kupanga bajeti kwa wakati unaofaa, kuzingatia vipaumbele vya Halmashauri na kuhakikisha kila Idara/kitengo kimeshirikishwa katika mchakato wa uandaaji wa bajeti. Lakini pia, wamejifunza namna ya kutengeneza mpangilio wa kazi unaowezesha kila hatua kufuatiliwa kwa wakati, na kuhakikisha mipango inatekelezwa kwa ufanisi.
Vilevile, washiriki wamepatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu kuandaa mipango na bajeti kwa mujibu wa viwango vya kitaifa, pamoja na mbinu za kupima maendeleo ya utekelezaji wake. Mafunzo hayo yamehimiza pia umuhimu wa kuhakikisha kila hatua inafuatiliwa ili kuepuka ucheleweshaji wa miradi ya Halmashauri na kupunguza makosa ya kifedha.
Hata hivyo, Maafisa Bajeti wamejadili changamoto zinazojitokeza katika uandaaji wa bajeti na mipango, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi, upungufu wa mafunzo ya mara kwa mara na rasilimali chache za kiutendaji. Wamekubaliana kuwa mafunzo kama haya yamekuwa muhimu sana kuongeza uelewa na uwezo wa Maafisa Bajeti.
Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Bajeti wenzake, Afisa TEHAMA Wilson Dossa, ameshukuru Idara ya Mipango na Uratibu kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu, huku akiomba yafanyike mara kwa mara ili kuwaimarisha zaidi.“Mafunzo haya yamekuwa muhimu sana kwetu, na tunatumai yataendelea kufanyika mara kwa mara, ili tuzidi kuimarika” amesema Dossa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa