Wananchi wa Vijiji vya Naunambe na Mbekenyera, vilivyopo Kata ya Mbekenyera, Wilaya ya Ruangwa, wamenufaika na elimu ya masuala ya kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, iliyofanyika leo, Februari 25, 2025.
Timu ya msaada wa kisheria imetoa elimu kuhusu sheria mbalimbali, ikiwemo haki za binadamu, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, sheria ya ndoa, sheria ya mirathi, na sheria ya ardhi. Pia, wananchi wamepata fursa ya kuwasilisha malalamiko na migogoro yao, ambapo wamepatiwa ushauri na ufafanuzi wa kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Wilaya ya Ruangwa, Antony Elias, amewahimiza wananchi kuhakikisha wanandikishana kisheria wanapouziana au kupeana ardhi ili kuepusha migogoro.
“Andikishaneni kisheria mnapouziana ama kupeana ardhi ili kuepusha migogoro, pia kakateni hati za ardhi zenu,” amesema Antony Elias.
Wananchi walioshiriki kampeni hiyo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopewa, wakisema itawasaidia kujua haki zao na kuepuka migogoro ya kisheria inayotokana na kutokujua taratibu sahihi. Wametoa pongezi kwa Serikali kwa kuanzisha kampeni hii yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikilenga kuwajengea wananchi uelewa wa sheria na kuwapa huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa