Wizara ya Katiba na Sheria imetoa mafunzo ya sheria, utawala bora, na haki za binadamu kwa Wakuu wa Idara, Vitengo, Kamati ya ulinzi na usalama na Watendaji wa Kata wa Wilaya ya Ruangwa, mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri leo, Machi 7, 2025.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha watumishi wa umma kuelewa misingi ya demokrasia, utawala bora, na haki za binadamu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Mada zilizotolewa zimejikita katika utawala wa sheria, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi, na umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu katika utendaji wa kazi za Serikali.
Aidha, Mgeni rasmi katika mafunzo hayo amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, ambaye ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo hayo, amesema kuwa elimu hiyo itaongeza ufanisi kwa watumishi wa umma na kuboresha utendaji kazi ndani ya Wilaya ya Ruangwa.
“Tumeyapokea mafunzo haya kwa mikono miwili na tuko tayari kujifunza na tunaamini uelewa wetu katika utawala bora na haki za binadamu utaimarika, jambo ambalo litasaidia katika utoaji wa huduma kwa wananchi kwa uadilifu na haki,” amesema Mhe. Ngoma.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Ndugu Moses Mayombo ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na usimamizi wa rasilimali watu, ameeleza kuwa mafunzo yamewapa mwanga kuhusu dhana ya utawala bora, umuhimu wa kufuata sheria, na namna ya kulinda haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza changamoto za kiutendaji zinazotokana na uelewa mdogo wa sheria na haki za wananchi.
Hapo awali, changamoto ya uelewa mdogo wa sheria, utawala bora, na haki za binadamu ilichangia matatizo katika utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo ucheleweshaji wa maamuzi na kutokuwepo kwa ushirikishwaji mzuri wa wananchi. Kupitia mafunzo hayo, watumishi wa umma wanatarajiwa kuwa na ufanisi zaidi, huku Serikali ikiendelea kutoa mafunzo zaidi ili kuhakikisha kila mtumishi anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwa kuheshimu haki za binadamu.
@katiba
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa