Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kwa mwaka 2025 inatarajiwa kuanza kesho, ambapo Wilaya ya Ruangwa itashiriki kikamilifu kwa kuendesha kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto mchanga.
Maadhimisho haya yatafanyika katika zahanati, vituo vya afya, hospitali pamoja na maeneo ya jamii, ambapo wahudumu wa afya wataelimisha wananchi juu ya umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita ya mwanzo bila kuongeza chakula kingine.
Aidha, tarehe 1 Agosti kutakuwa na kipindi maalum kupitia Redio Ruangwa saa 12 jioni, ambacho kitawahusisha wataalamu wa afya wakitoa elimu, kuhamasisha unyonyeshaji, na kujibu maswali ya moja kwa moja kutoka kwa wasikilizaji.
Vilevile, wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika shughuli zitakazoandaliwa katika maeneo yao, ikiwemo mikutano midogo ya uelimishaji, kuangalia video fupi za kielimu, na kusikiliza vipindi vya redio vitakavyowasilisha ushuhuda wa kina mama waliowahi kufaidika na unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Kwa ujumla, Wiki ya Unyonyeshaji huadhimishwa duniani kote kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti ya kila mwaka kwa lengo la kuunga mkono afya ya mama na mtoto, kupunguza vifo vya watoto wachanga, na kuhimiza jamii kushiriki katika ulinzi wa haki ya mtoto kupata maziwa ya mama.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa