Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua mradi wa usambazaji maji kwenye vijiji vinavyopitiwa na mradi wa maji ya Mbwinji na ameridhishwa na unavyoendelea.
Mradi huo unaosimamiwa na mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira Masasi, Nachingwea(MANAWASA) unatarajiwa kukamilika machi 31,2018.
Waziri Mkuu alifanya ukaguzi huo alipofanya ziara yake ya kikazi Wilayani Ruangwa katika kioksi cha kuchotea maji kilichopo kwenye kijiji cha Mbecha Wilayani Ruangwa.
“Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya tano, hivyo vijiji vyote vitapata maji” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema vijiji ambavyo vimenufaika na mradi huu Wilayani Ruangwa ni sita ambavyo ni Chiapi, Nandanga, Ipigo, Luchelegwa, Litama na Mbecha.
Amesema serikali ya awamu ya tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye tatizo hilo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA Mhandisi David Mwamsojo alisema mradi huo utagharimu sh. Milioni 870.738 hadi kukamilika.
Amesema mradi huo unahusisha vijiji 12 vilivyo kwenye umbali wa kilomita tano kutoka kwenye bomba kuu pamoja na ujenzi wa vioski 18 vya kuchotea maji.
Mhandisi Mwamsojo amesema hadi sasa tayari kazi ya ulazaji mabomba na kuweka vituo 16 vya kuchotea maji katika vijiji 11 vinavyonufaika na mradi huo imekamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama.
Alitaja vijiji hivyo kuwa ni Mtepeche, Magereza, Mailisita, Mkotokuyana na Naipanga vya Wilaya na Nachingwea na Chiapi, Nandanga, Ipigo, Luchelegwa, Litama na Mbecha vya Wilaya ya Ruangwa
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa