WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi pikipiki 100 zenye thamani ya sh. milioni 260 kwa vijana wa wilaya ya Ruangwa ili wazitumie kufanya biashara ya usafirishaji.
Akizungumza na vijana wa Ruangwa kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya CWT, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema utoaji wa pikipiki hizo ni muendelezo wa mpango wa ofisi ya Mbunge wa kuwawezesha vijana, wanaume, wanawake na wazee.
"Mwaka 2016/2017 tulichukua pikipiki 235 na kuzigawa kwenye wilaya yote hii. Na jambo zuri kwa sasa, kwenye Serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania na yeye ameamua kuwa na kada ya wasafirishaji wa wadogo, wa kati na wakubwa.”
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa aliwaeleza vijana hao watambue kwamba na wao ni wasafirishaji wa usafiri wa kawaida kwa kutumia pikipiki.
Mapema, akielezea mradi huo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Bw. Martin Mbwana alimweleza Waziri Mkuu kwamba pikipiki hizo zitakopeshwa kwa bei ya sh. milioni 2.6 bila riba yoyote na kwamba muda wa marejesho ni miezi nane.
“Kuanzia sasa hadi Desemba, mwaka huu mtu anapaswa awe amekamilisha mkopo wake. Na kianzio ni kati ya sh. 500,000 hadi 700,000. Mkopo huu umetolewa chini ya mdhamini mkuu, Bw. Mpaluka Hashim Mtopela,” alisema.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya biashara na kuongeza: “Nikiwa mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa soko la Kariakoo, niko hapa Ruangwa ili kuwawezesha vijana wa Ruangwa,” alisema.
Kwa upande wake, mdhamini mkuu wa pikipiki hizo, Bw. Mpaluka Hashim Mtopela alimshuruku Waziri Mkuu kwa kuamua kuwajali vijana wa jimbo lake. “Mwaka 2016 ulitoa pikipiki 235 ambazo zimewesha vijana zaidi ya 600 kuishi maisha mazuri wao na familia zao. Wako waliopewa pikipiki moja lakini leo hii wanamiliki pikipiki tatu hadi nne.”
“Hii ina maana leo tukimpa kijana sh. milioni 2.6, baada ya muda ataweza kutengeneza shilingi milioni 7. Vijana hawa nimewachukulia dhamana kwa sababu ninaamini wanaweza kuzirejesha. Safari hii tumechukua pikipiki lakini muda ujao tutachukua mashine ya kufyatulia matofali au ya kumwagilia bustani kwa sababu tunao vijana wenye uwezo,” alisema.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa