Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Seleman Jafo, ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ruangwa, amesema kuwa juhudi zinazofanywa wilayani humo zimepita matarajio, akiwa katika ziara ya kikazi leo, Septemba 20, 2024, Waziri Jafo amekagua miradi kadhaa na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.
Miongoni mwa miradi aliyoikagua ni ujenzi wa barabara ya Mipingoni, ambayo itaimarisha upatikanaji wa huduma na kuchochea maendeleo ya uchumi kwa wananchi. Pia, ametembelea ghala la kuhifadhia mazao la Lipande, ambalo limejengwa kwa lengo la kusaidia wakulima katika kuhifadhi mazao yao kwa muda mrefu na kwa ubora.
Aidha, Mhe. Jafo ametembelea Shule ya Msingi Likangara, ambayo imejengwa kwa thamani ya Shilingi Milioni 500 za Kitanzania, shule hiyo ya ghorofa ina madarasa nane, ofisi nne za walimu, na matundu 24 ya vyoo, ikiwa ni hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya elimu katika wanafunzi, Mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa shule kupokea wanafunzi wengi zaidi na kutoa elimu bora.
Waziri Jafo pia ametembelea Chuo cha Ufundi (VETA) Nandagala, ambacho kinatarajiwa kuwa kitovu cha kuwapa vijana wa Ruangwa ujuzi wa kitaalamu ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda. Lakini pia ametembelea mradi wa maji wa Chimbila "A" ambao unatarajiwa kunufaisha vijiji 34 na kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Ikumbukwe, kwamba katika miaka ya hivi karibuni, jitihada za Serikali zimeleta matokeo chanya makubwa, na Wilaya ya Ruangwa sasa inashuhudia mafanikio makubwa kimaendeleo, Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa miradi na kuboresha miundombinu kwa ufanisi, huku ikihakikisha kuwa sekta muhimu kama elimu na maji zinapata uwekezaji wa kutosha kwa maendeleo endelevu ya wananchi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa