Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey zambi, amewataka Wazazi kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ili kuleta matokeo chanya katika ufaulu wa wanafunzi Wilayani humo.
Zambi ameyasema hayo siku jana katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika kata ya makanjiro na Likunja alipotembelea na kukagua maendeleo ya shule ambapo alikagua pia maandalio ya walimu na kuangalia maendeleo ya wananfunzi katika shule za msingi, Mbangara, Chikoko, Chilangalile ikiwa ni ziara yake ya kikazi.
Zambi amesema wazazi wanajukumu la kuwasaidia walimu katika kuongeza ufauli kwa kukagua madaftari ya wanafunzi na kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni na kuhakikisha wanakuwa na maadili mema .
“Watoto wa siku hizi unamkuta mtoto wa kidato cha kwanza au msingi anamiliki simu na mzazi ajui simu hiyo mtoto wake ameitoa wapi, wazazi zuieni matumizi ya simu kwa watoto wenu wadogo na mfuatilie wanazitoa wapi” amesema Zambi
“Ruangwa ya ufaulu inawezekana, Ruangwa bila mimba za utotoni inawezekana , Ruangwa bila utoro mashuleni inawezekana na haya yote yatawezekana kwa ushirikiano wa walimu wa wanajamii”.amesema zambi
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Joseph Mkirikiti amewataka walimu kuipenda na kuifanya kazi yao kama ni wito na kutimiza majukumu yao ili kutoka katika kipindi hiki kibovu cha ufaulu mbaya Wilayani humo katika shule za msingi na sekondari.
“Ni aibu sana Wilaya kama hii anayotoka Waziri Mkuu kuwa tunafanya vibaya ni wakati wa mabadiliko sasa kila mtu ajiangalie na kujitahimini kwani suala la elimu linamgusa kila mtu” amesema Mkirikiti.
Naye Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Ruangwa Selemani Mrope amesema wako tayari kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na mkuu huyo wa mkoa ili kubadilisha hali ya ufaulu wa wanafunzi
“Katika kuhakikisha tunafanikiwa Idara ya elimu msingi itafanya msawazo wa walimu kutokana na mahitaji yaliyopo katika baadhi ya shule, na tutawafuatilia mashuleni ili kuangalia maandalio wanayoyaandaa kama wanayafuata.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa