Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbekenyera iliyopo Kata ya Mbekenyera wilayani Ruangwa Answabu Abdallah Maloi (13) ametoa wito kwa wazazi na walezi kutowakataza watoto wao kuonesha na kukuza vipaji vyao kikubwa ni kuzingatia usalama wao.
" Watoto tuna vipaji vingi lakini kuna wakati wazazi/ walezi wanatukatisha tamaa na kutufanya vipaji vyetu tusivioneshe kabisa, hivyo basi niwaombe wazazi pindi mnapogundua watoto wenu tuna kitu/ kipaji fulani msituzuie kukionesha na kukikuza pia kwasababu kipaji hicho inaweza ikawa njia ya mafanikio yetu, na watoto tukifanikiwa na nyinyi wazazi mnafanikiwa, kikubwa zingatieni usalama wetu na kukiamini kile tunachokifanya" amesema Answabu
Ameyasema hayo leo Julai 8, 2024 kupitia Redio Jamii, Ruangwa Fm katika kipindi cha "Bodaboda" kinachoongozwa na Mtangazaji Adelina Kaspari.
Mwanafunzi Answabu ameshiriki katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania 2024 (UMITASHUMTA) kupitia mchezo wa mpira wa miguu kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa na amechaguliwa katika timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17.
Aidha, Answabu ameongeza kwa kusema kuwa mtu yeyote unapofanya jambo usilewe sifa unazopewa na watu wengine kwa mara ya kwanza kikubwa ni kuongeza juhudi ili wakusifie zaidi unavyofanya jambo kubwa na zuri kwako wewe mwenyewe na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Afisa Michezo Wilaya Ndugu Shaban Mchinama amewashukuru wazazi wa Answabu kwa kumruhusu mtoto wao kushiriki katika michezo na kutoa wito kwa wazazi wengine waige mfano huu kwani michezo ni afya, urafiki na ajira.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa