Watumishi wa ajira mpya katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Watumishi Portal (e-Utendaji) unaowezesha usimamizi na upimaji wa utendaji wao wa kazi.
Mafunzo hayo yamefanyika Februari 12, 2025, yakiongozwa na Kinara wa Mfumo wa Watumishi Portal kwa Mkoa wa Lindi, Ndugu Mohamedi Hamisi Mohamedi, kwa kushirikiana na Maafisa Utumishi wa Wilaya, mfumo huo unalenga kurahisisha upimaji wa utendaji wa kazi kwa watumishi wa umma kwa kuhakikisha taarifa zao zinapatikana kwa urahisi na kwa uwazi.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utawala na usimamizi wa rasilimali watu, Ndugu Frank Edger Komba, amesema mfumo huo ni muhimu katika kusimamia uwajibikaji wa watumishi.
“Mfumo huu unatoa fursa ya kutathmini utendaji wenu kwa uwazi na kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi, ni muhimu kuutumia ipasavyo ili kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Ndugu Komba.
Kadhalika, Ndugu Mohamedi Hamisi Mohamedi ameongeza kuwa mfumo huo utarahisisha utendaji wa kazi kwa kuhakikisha kila mtumishi anajisajili na kurekodi shughuli zake za kila siku.
“Watumishi wenzangu mnapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya mfumo huu ili kurahisisha usimamizi wa rasilimali watu na kupima utendaji wanu kwa uwazi,” amesema Mohamedi.
Naye, Mmoja wa watumishi wapya Bi. Consolata Macha, ambaye ni mtendaji wa kijiji cha Lipande, amesema kuwa mfumo huu umemsaidia kuelewa jinsi ya kuweka taarifa zake za utendaji kazini.
“Awali sikujua jinsi ya kuripoti kazi zangu kwa njia rasmi, lakini kupitia mafunzo haya nimejifunza namna mfumo unavyofanya kazi na umuhimu wake,” amesema Bi. Macha.
Hata hivyo ni muhimu kutambua kwamba, Kabla ya mfumo wa e-Utendaji, upimaji wa utendaji wa watumishi ulifanyika kwa njia za kawaida, jambo lililokuwa likisababisha ucheleweshaji wa tathmini, lakini kwa sasa mfumo huu unarahisisha upimaji wa utendaji kwa uwazi zaidi. Serikali inatarajia kuwa matumizi sahihi ya mfumo huu yataongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuboresha utoaji wa huduma.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa