Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuuheshimu na kuuendeleza utamaduni ambao ndio urithi wao ili kulifanya Taifa liendelee kuwa hai.
Amesema suala la kuuenzi utamaduni ni jambo zuri ambalo linatoa fursa kwa watu wengine hususani wa mataifa ya nje kuja kujifunza historia ya Watanzania na maisha yao.
Waziri Mkuu aliyasema hayo (Ijumaa, Oktoba 26, 2018) alipotembelea shughuli za tamasha la utamadini wa Mtanzania kwa jamii ya watu wa Lindi.
Katika tamasha hilo linalofanyika kwenye Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania waendelee kuupenda utamaduni wao.
“Nimefurahi kuona nyumba zikiwa na zana mbalimbali za kitamaduni ambazo zilikuwa zikitumiwa na wazee wetu pamoja na namba ya utayarishaji wa vyakula vyetu vya asili.”
“Sikutarajia kuona haya ninayoyaona, nawashukuru wote walioshiriki katika kandaa tamasha hili pamoja na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Kijiji cha Makumbusho.”
Waziri Mkuu alisema tamasha hilo ambalo limewakutanisha Wanalindi kutoka katika wilaya mbalimbali linatoa fursa ya wao kujadili maendeleo ya mkoa wao na Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wote wajitokeze kwa wingi kwenda katika Kijiji cha Makumbusho kwa ajili ya kujifunza historia ya mkoa wa Lindi pamoja na fursa zilizoko.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema mkoa umetumia tamasha hilo kutoa ujumbe kwa umma kuhusu vivutio mbalimbali walivyonavyo pamoja na fursa za uwekezaji.
(mwisho)
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa