Jumla ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi 44 Jimboni Ruangwa wa ngazi ya kata wamekula viapo rasmi vya utii na kutunza siri, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Octoba 2025.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika leo tarehe 04 Agosti 2025 katika ukumbi wa Shule ya Wasichana Ruangwa, ikiongozwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Jonas Munguatosha Lyakundi, mbele ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo.
Katika kiapo hicho, wasimamizi hao wameapa kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni za uchaguzi, pamoja na miongozo rasmi inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha, kiapo cha kutunza siri kimelenga kuhakikisha kuwa wasimamizi hao hawatafichua taarifa au nyaraka zozote za uchaguzi bila idhini ya kisheria, hali inayolenga kulinda usalama wa taarifa na uhalali wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwl. Mbesigwe ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo amewataka wasimamizi hao kutambua uzito wa kiapo walichokula na kuwa waaminifu kwa taifa.
“Mmekula kiapo mbele ya umma na mbele ya sheria sasa jukumu lenu ni kulinda imani ya wananchi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa vitendo,” amesema Mwl. Mbesigwe.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, kila msimamizi anapaswa kula kiapo rasmi cha fomu namba 6 na 7 kabla ya kuanza majukumu yake ili kuthibitisha dhamira ya kutekeleza wajibu kwa haki na bila upendeleo. Zoezi hilo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika mchakato wa uchaguzi.
Wasimamizi hao 44 wanatarajiwa kusimamia shughuli zote za uchaguzi katika kata 22 za Jimbo la Ruangwa, ambapo kila kata itakuwa na wasimamizi wawili waliopata mafunzo na sasa wameshatimiza masharti ya kiapo cha kisheria.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa