Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Ruangwa wameapishwa rasmi leo Oktoba 26, 2025, wakitakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uzalendo na kufuata sheria zote za uchaguzi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi hao, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ruangwa, George Mbesigwe, amesema watendaji hao hawapaswi kuwa chanzo cha malalamiko bali wawe walinzi wa haki, amani na uhalali wa matokeo ya uchaguzi.
“Msimamizi wa kituo anatakiwa kuwa mfano wa uadilifu. Msikubali kuwa sababu ya malalamiko au vurugu. Fanyeni kazi kwa weledi, kwa kufuata sheria na taratibu zote za uchaguzi,” amesema Mbesigwe, akisisitiza umuhimu wa kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi.
Aidha, Mbesigwe amesema wapiga kura wenye mahitaji maalum wanapaswa kupewa kipaumbele siku ya kupiga kura, Oktoba 29, 2025, ili kuhakikisha ushiriki wa makundi yote katika mchakato wa kidemokrasia.
Kwa upande mwingine, mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika Oktoba 26 na 27 yamegawanywa katika Tarafa tatu za Wilaya ya Ruangwa Tarafa ya Mnacho (Chuo cha VETA), Tarafa ya Ruangwa (Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa), na Tarafa ya Mandawa (Shule ya Sekondari Mbekenyera).
Vilevile, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wasimamizi na wasaidizi wao ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani, uwazi na bila upendeleo, sambamba na kuhakikisha kila kura inahesabiwa kwa mujibu wa sheria.
Mbali na hilo, wasimamizi hao wameapishwa kwa kiapo cha kutunza siri na wamepatiwa mafunzo ya maadili ya kazi, huku wakitakiwa kutoa tamko la kujitoa au kutojihusisha na chama chochote cha siasa kabla ya kusimamia mchakato wa upigaji kura.
Kwa mujibu wa Mbesigwe, jumla ya wasimamizi na wasaidizi 1,211 watasimamia vituo 389 vilivyopo katika kata 22 za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Sambamba na hayo, Mbesigwe amesema maandalizi hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wa Ruangwa wanatekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani na utulivu, huku akitoa wito kwa watendaji hao kulinda misingi ya haki, uadilifu na uwazi katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa