Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo vya Kupigia Kura wilayani Ruangwa wameanza rasmi mafunzo yao kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unafanyika kwa haki, amani, na utulivu, mafunzo hayo yamefunguliwa leo Novemba 23, 2024 na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, Ndugu Frank Fabian Chonya, katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Nkowe, Tarafa ya Mnacho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Ndugu Chonya amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi, akiwataka kushiriki kwa umakini mkubwa, ameeleza kuwa mafunzo haya ni msingi wa kufanikisha uchaguzi wa haki na yanatoa fursa kwa washiriki kuuliza maswali ili kujenga uelewa wa kina kuhusu majukumu yao.
“Mnapaswa kuwa watii, wazalendo, na kufuata sheria na kanuni za kazi hii muhimu kwa Taifa, kiapo mlichokula kinapaswa kuwa mwongozo wenu mnapotekeleza majukumu haya,” amesema Ndugu Chonya, akiwakumbusha wahusika umuhimu wa uadilifu katika utekelezaji wa kazi hiyo.
Katika mafunzo hayo, Wasimamizi wameelekezwa taratibu mbalimbali za uchaguzi, ikiwemo usimamizi wa upigaji kura, kuhesabu kura, na kutangaza matokeo. Pia, mifano ya karatasi za kupigia kura na fomu za matokeo zilifanyiwa kazi kwa vitendo, huku washiriki wakishiriki majadiliano ya pamoja ili kuboresha uelewa wa mchakato mzima.
Aidha, Ndugu Chonya ametoa barua za uteuzi kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa vituo vya kupigia kura, hatua inayowapa mamlaka rasmi ya kutekeleza majukumu yao ifikapo Jumatano, Novemba 27.
Kwa kumalizia, amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kutanguliza uzalendo na kuzingatia taratibu ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kuleta matokeo yenye tija kwa jamii ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa