Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Bi Rose Reuben amewataka wanawake wa Ruangwa kubadilika kwa kupinga kuishi katika maisha ya ukatili wa kijinsia.
Pia amewataka wazazi kuacha kuwanyima haki ya mtoto kupata elimu kwani ni jukumu la mzazi kumpatia mtoto elimu na si kumshawishi afanye vibaya katika mitihani yake ya mwisho.
Amesema hayo leo Machi 29/ 2019 wakati wa mkutano wa wadau kujadili mbinu/mkakati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika ukumbi wa Rutesco Ruangwa mjini.
Bi Rose amesema lengo la TAMWA ni kusaidia jamii kuondokana na changamoto za ukatili wa kijinsia hivyo wataendelea kuhakikisha changamoto hizo zinaisha katika jamii ya Ruangwa
"Suala la kupinga ukatili wa kijinsia si la TAMWA pekee yake ni jukumu la kila mwananchi hivyo tusaidiane kubainisha changamoto hizo na sisi tutasimamia kutoa elimu katika kuhakikisha tunatokomeza hizo changamoto"amesema Bi Rose.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hashim Mgandilwa ametoa rai kwa wananchi wa Ruangwa kuacha kuwahamasisha watoto kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ya darasa saba na kidato nne.
Mheshimiwa Mgandilwa amesema mzazi atakayebainika anafanya jambo la kushawishi mtoto afeli kwa kisingizo cha kukosa uwezo wa kusomesha atamchukulia hatua za kisheria.
Pia amewataka wazazi wa Ruangwa kubeba majukumu yao kama wazazi kwa kuwasimamia watoto wao katika mienendo iliyobora na kuwahamasisha watoto hao kufanya vizur katika masomo yao.
Pia alitoa rai kwa uongozi wa TAMWA kusaidia kutatua changamoto zilizobainishwa na wadau ili kumaliza matatizo yanayowakabili watoto na wanawake.
"Nitoe shukurani za dhati kwa jitihada mnazozifanya TAMWA na nitapenda sana siku mkiniambia nije nizindue bweni mlilojenga kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotembea umbali mrefu hasa wa kike" amesema Mgandilwa.
Vile vile mjumbe Esha Issa amesema wanaochangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto ni wamama wenyewe kwani wamekuwa ndiyo watu wenye sauti kubwa katika familia na wanaitumia sauti hiyo vibaya.
"Wamama hatutaki watoto wetu wasemwe wakikosea hata ukiletewa mashitaka ya mtoto anafanya uhuni unakuwa mkali utaki kuamini na hata akipata mimba unaishia kusema acha aongeze dunia"amesema
Hili ni tatizo sana kwani watoto wetu wanakuwa hawana adabu na wanapata nguvu ya kufanya mambo ya ajabu kwasababu anaona mzazi mwenyewe unafurahia ujinga anaoufanya.
Hata hivyo aliushukuru uongozi wa TAMWA na aliuomba uongozi huo kutoa elimu ya madhara ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wa ngazi ya kata na vijiji mara kwa mara ili kimaliza matatizo hayo katika jamii ya Ruangwa.
(MWISHO)
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa