Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Ndg, Frank Chonya amewaagiza watendaji wa vijiji vya Mkutingome na Namilema kuwafuatilia wanafunzi 28 wa darasa la saba ambao hawajaripoti katika kituo chao cha kambi Naunambe.
Ametoa tamko tarehe 31/08/2020 alipofanya ziara ya kutembelea kambi mbilii ya Naunambe na Mbekenyera zilizopo katika kata ya Mbekenyera.
Aidha, Mkurugenzi alimtaka Mkuu wa shule ya Naunambe kuacha kutoa ruhusa zisizo za lazima kwa wanafunzi hao wa darasa saba kwani kufanya hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi hao,
“Tuna malengo yetu na ni lazima tuyafikie hatuwezi kuyafikia kama tutaendelea na utaratibu huu, tumekubaliana kufika asilimia 100 ya ufaulu kitaifa ili tufike hapo wanafunzi kwa pamoja ni lazima wahudhurie darasani siku zote za kambi” amesema Chonya
Pia Mkurugenzi Chonya aliahidi kuwa kambi itakayofaulisha vizuri itazawadiwa shilingi laki mbili kama motisha yao na mwalimu mkuu wa shule ilipo kambi atapata motisha ya shilingi elf arobaini.
"Hizi ni ahadi ambazo nitatimizia mwenyewe bila shida yoyote, hivyo fundisheni wanafunzi wetu wafaulu mpate hizo fedha fanyeni mabadiliko walimu tusomeke kitaifa katika kumi bora” amesema Chonya.
Vile vile Ndg Chonya amewashauri walimu wakuu wa shule za Ruangwa kuchangia kiasi cha shilingi laki moja kutoka katika fedha zao za posho ya madaraka kwa ajili ya kuwanunulia chakula walimu wanaojitolea katika makambi.
“Halmashauri imetoa chakula kwa ajili ya walimu hao si vibaya na wakuu wa shule wakaonyesha uzalendo, mwalimu anapaswa asiwaze wala asiwe na shida ya chakula ili ufundishaji wake uzidi kuimarika” amesema Chonya.
Naye Mratibu elimu kata Jofrey Robert Manase ameushukuru uongozi wa kijiji cha Mbekenyera kwa kuwapa ushirikiano katika kambi ya Mbekenyera kwa kuwavutia umeme katika madarasa wanayosomea wanafunzi hao.
Mratibu huyo kwa niaba ya walimu waliopo katika kambi ya Naunambe na Mbekenyera alimuhakikishia Mkurugenzi Kuwa watafanya vizuri na kufikia malengo ya asilimia mia ufaulu kitaifa.
Wilaya ya Ruangwa ina jumla ya kambi 21 ambazo zipo katika shule zote zilizopo ndani ya Ruangwa.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa