WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wabadilike na watafakari namna bora ya kuboresha maisha yao na wafanye kazi kwa bidii badala ya kukaa vijiweni na kulalamika.
Amesema kama kuna changamoto zinawakabili katika utekelezaji wa shughuli zao, basi watumie njia sahihi ikiwemo kuwasiliana na viongozi husika waliopo kwenye maeneo yao.
Aliyasema hayo jana jioni wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nandagala, wilayani Ruangwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye zahanati ya kijiji cha Nandagala.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mary Majaliwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa, alisema vijana wanatakiwa kujitambua na kuiunga mkono Serikali kwa kufanya kazi kwa bidii.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka vijana washirikiane kwa pamoja katika kubuni shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato, jambo ambalo litawakwamua kiuchumi na kuwawezesha kujitegemea.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao mikakati mbalimbali inayofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo ya wilaya hiyo ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya pamoja na maji safi na salama.
PiaWaziri Mkuu aliwataka wananchi hao waendelee kuiunga mkono Serikali yao, ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
(mwisho)
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa