Jamii imeshauriwa kushirikiana kwa umoja wao ili kupunguza tatizo la ukatili wa kijinsia katika jamii ya wananchi wa Ruangwa
Ushauri huo umetolewa mwenyekiti wa kijiji cha Mtondo Bakari Nanyambo kilichopo kata ya Nambilanje wakati wa mdahalo wa wanakijiji kuhusu mila na desturi zinazopelekea madhara katika kijiji cha Mtondo leo 02/04/2019 unaoendeshwa na Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA)
Alisema Mwenyekiti kuwa watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kiwango cha juu na kesi nyingi haziendi mbele sababu nyingi humalizwa kifamilia jambo ambalo si sawa kwani mtoto anakuwa ameshaharibiwa.
“Mtoto akishazoeshwa michezo ya ukatili wa kingono tunazalisha kizazi kisichoeleweka na ukifuatilia chanzo cha tatizo ni mazingira mabovu ya nyumbani, hivyo tusipounganisha nguvu zetu pamoja kizazi chetu kwa asilimia kubwa kitakuwa kisicho na elimu ni jukumu letu kuhakikisha hili linadhibitiwa mapema kabla ya kuleta athari kubwa kwa jamii.”Alisema Nanyambo
Hata hivyo alisema kuwa ukatili wa kijinsia huanzia kwa asilimia kubwa katika malezi kwani kuna watoto ambao hufanyiwa ukatili wanashindwa kuwashirikisha wazazi na hata wanapowashirikisha wazazi wanaona aibu kupeleka kesi katika ofisi ya serikali ya kijiji hivyo kupelekea tatizo kuwa kubwa na kumuathiri mtoto.
“Lazima tuweke utaratibu wa kutoa elimu ya makuzi ya vijana na ndio maana shuleni tumeweka walimu wanaoshughulikia matatizo ya watoto wa kike na kiume na kutenga sehemu maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujistiri na yote yanafanyika ili kupambana na ukatili wa kijinsia nchini.”Alisisitiza Nanyambo
Kwa upande wake mkazi wa Mtondo Hamisi Mbinga Unyago amesema chanzo kikibwa ni kuwa kuendekeza mila ambazo ni zakizamani hivyo ameiomba serikali kuweka sheria ya umri wa mtoto kuchezwa unyago ili kumaliza tatizo la mimba za utotoni na watoto hasa wa kike kuacha masomo njiani.
Pia aliwaomba wanaume wenzie kuacha kutelekeza wanawake walioza nao inasababisha watoto kuishi maisha ya shida yanayopelekea mtoto huyo kukosa haki yake ya kupata elimu na malezi bora ya baba na mama na hili si kwa kinababa tu hata kinamama mnaowakuta watoto wa mume zenu usiwanyanyase hao watoto wapeni malezi bora ili tutokomeze suala la ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Pia aliuomba uongozi wa serikali ya kijiji kuendelea kuwapa mafunzo kama haya yanayotolewa na TAMWA kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujua athari ya vitu wanavyovifanya inavyowaathiri sana watoto wakike kwani walikuwa hawajui hata kama kilimo cha kuhamahama kinaweza kuwa na madhara kwa watoto wao.
(MWISHO)
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa