Kambi maalum ya upasuaji wa macho iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi imeokoa mamilioni ya fedha kwa wananchi waliokuwa wanakabiliwa na matatizo ya macho, hususan mtoto wa jicho, Kambi hiyo iliyofanyika kati ya Julai 8 mpaka Julai 19, 2024, imewasaidia wagonjwa 270 kupata upasuaji wa bure, hatua ambayo imewaepusha na rufaa kwenda hospitali kubwa kama Muhimbili.
Huduma hiyo imetokana na ushirikiano kati ya taasisi ya madaktari wa macho kutoka Marekani, Eyecops, na Serikali ya Tanzania, na imeleta matumaini kwa wakazi wa Ruangwa ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto za kukosa huduma hizo ndani ya Wilaya yao.
“Tumeokoa Maelfu ya Shilingi kwa Wananchi”
Dkt. Mwita Machage, mratibu wa huduma za macho mkoani Lindi, amebainisha kwamba upasuaji huo umeleta nuru kwa wananchi wengi. “Tumefanikiwa kufanya upasuaji wa macho kwa watu 270 ambao wengi walikuwa wamepoteza uwezo wa kuona kutokana na mtoto wa jicho. Kama wangetakiwa kwenda Muhimbili, kila mmoja angehitaji kutumia zaidi ya shilingi milioni mbili kwa matibabu, usafiri, na malazi,” amesema Dkt. Machage, akieleza kuwa huduma hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kifedha kwa familia nyingi.
Aidha, Dkt. Machage amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kujitokeza kwa uchunguzi wa macho mapema ili kuepuka matatizo makubwa yanayoweza kuzuilika.
“Huduma Iliyopunguza Rufaa na Kuweka Nafuu kwa Jamii”
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Feisal Said, amepongeza huduma hiyo kwa kusaidia kuepusha rufaa za mara kwa mara kwenda hospitali kubwa. “Awali, wagonjwa wengi walikuwa wakilazimika kwenda hospitali za mbali kwa ajili ya upasuaji wa macho. Lakini kupitia kambi hii, wananchi wengi wameweza kupatiwa matibabu hapa wilayani, bila gharama za usafiri au matibabu,” amesema Dkt. Said, akielezea jinsi kambi hiyo ilivyosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya macho kituoni.
Upasuaji Ulivyosaidia Wagonjwa Kituo cha afya Ruangwa
Dkt. Isack Nonga, Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ruangwa, ameongeza kuwa kambi hiyo imesaidia sana katika kupunguza msongamano wa wagonjwa wenye matatizo ya macho kituoni hapo. “Tulikuwa tunapokea wagonjwa wengi walioathirika na mtoto wa jicho, na hatukuwa na vifaa vya kuwahudumia. Sasa, idadi ya wagonjwa imepungua sana, na wengi wamepona kabisa baada ya upasuaji,” amesema Dkt. Nonga.
“Wananchi Wanatamani Kambi Hii Irejee Tena”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Chonya l, amesema kuwa mafanikio ya kambi hiyo yamepokelewa kwa shangwe na wananchi, ambao sasa wanaomba huduma kama hizo zirejee mara kwa mara. “Kambi hii imeokoa fedha nyingi kwa familia nyingi, na wengi wanatamani huduma hii iendelee,” amesema Chonya, akiashiria jinsi ambavyo huduma hiyo imekuwa mkombozi kwa jamii ya Ruangwa.
Chonya pia amepongeza juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya afya, akisisitiza kuwa mafanikio haya ni sehemu ya mipango ya serikali kupeleka huduma muhimu za afya vijijini.
Wananchi Wafurahia Huduma Hii
Raia mbalimbali wameeleza furaha yao kutokana na huduma hii muhimu. Bw. Ally Kondo (60), kutoka Kijiji cha Chienjele, amesema, “Nilikuwa na tatizo la macho kwa miaka mingi, lakini sasa naweza kuona vizuri. Tunaomba huduma kama hizi zirejee mara kwa mara ili kusaidia watu wengi zaidi, ninamshukru sana mama Samia na wasaidizi wake kwa kutujali sisi wannchi wanyonge.”
Bi. Zainabu Thomas (68), mkazi wa kijiji cha Kipindimbi, naye amesema, “Kwa miaka miwili sikuweza kuona vizuri, lakini sasa nimepona baada ya kufanyiwa upasuaji, vijijini kunq watu wengi sana wenye matatizo ya macho wasiokuwa na uwezo wa kifadha, viongozi wazalendo kama mama Samia wakileta huduma kama hizi kwetu wanyonge sisi malipo yetu ni kuwaombea dua kwa Mungu tu. Tunaomba kambi kama hii ziletwe kwa wingi vijijini.”
Mafanikio ya kambi ya upasuaji wa macho katika Wilaya ya Ruangwa yameleta matumaini makubwa kwa wakazi wa Ruangwa, ikionyesha jinsi huduma za afya zinavyoweza kuboresha maisha ya watu vijijini na kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia nyingi. Wananchi wengi wamepata fursa ya kurejesha uwezo wao wa kuona, hatua iliyoboresha maisha yao na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Huku zaidi ya watu mia sita wakifanyiwa uchunguzi wa macho, ni dhahiri kwamba huduma hii imekuwa mkombozi kwa jamii. Wananchi wanaiomba Serikali na wadau kuendelea kuleta huduma kama hizi mara kwa mara ili kuhakikisha matatizo ya macho na magonjwa mengine yanapatiwa ufumbuzi mapema. Hatua hizi sio tu zinaboresha afya ya jamii, bali pia zinachangia kujenga taifa lenye nguvu kazi bora, linalojikita katika ustawi na maendeleo endelevu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa