Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemuagiza Mkandarasi wa kampuni ya M/s China Railway 15 Bureau Group Cooperation kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa Daraja la Lukuledi ndani ya miezi mitatu, agizo hilo ametoa leo tarehe 11 Januari 2025 wakati akikagua maendeleo ya Barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga (KM 106).
Waziri Ulega amesisitiza kuwa fedha za mradi huo zipo, na hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuongeza kasi ili wananchi wa Nachingwea na Ruangwa wanufaike na miundombinu hiyo. Aidha, ameagiza kuwa barabara hiyo iwe na taa za barabarani ili kuimarisha usalama, kuchochea ukuaji wa miji, na kuongeza fursa za biashara kwa wananchi.
Naye, Msimamizi wa mradi kutoka TECU, Mhandisi Simon Makala, amesema jumla ya wakazi 165 wa eneo la Ruangwa wamepata ajira za muda mfupi kupitia mradi huo, na ameongeza kuwa utaratibu huo utaendelea kadri kazi zinavyosonga mbele.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mohamed Moyo, amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara na madaraja kwa kuepuka vitendo vya uharibifu kama wizi wa alama za barabarani na uchimbaji wa mchanga pembezoni mwa barabara.
Ikumbukwe, Barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga ni barabara ya kimkakati yenye urefu wa kilomita 106, ambayo ujenzi wake umegawanywa katika sehemu mbili: Nachingwea-Ruangwa (KM 57.6) na Ruangwa-Nanganga (KM 53.2). Kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua mtandao wa barabara mkoani Lindi na kuchochea uzalishaji wa mazao kama ufuta, mbaazi, korosho, na alizeti, hivyo kuinua uchumi wa wananchi wa Nachingwea na Ruangwa, pamoja na kuboresha sekta ya usafirishaji.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa