Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya Uchumi Profesa Bernadeta Killiani amesema kwamba Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam tawi la Ruangwa watahakikisha ndani ya miezi 18 Mkandarasi anakabidhi majengo.
Ameyasema hayo leo Julai 9, 2024 katika Kikao kazi cha uzinduzi wa Kamati ya "Kasema" itakayoshirikiana na Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya Uchumi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri.
Aidha, Profesa Killiani ametoa wito kwa wananchi wa Ruangwa kuonesha ushirikiano kwani mafanikio ya Mradi yanategemea muamko na ushirikiano na wanachi wa eneo husika.
Kamati ya "Kasema" ina Wajumbe watano na ina lengo la kukusanya na kushughulikia maoni au malalamiko ya wananchi katika eneo husika kuhusu Mradi.
Pia, ina lengo la kuweka kumbukumbu za kile kinachofanyika katika Mradi, na ni sehemu ya Ulinzi na Usalama wa Mradi huo.
Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya Uchumi chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam umefadhiliwa na Mkopo wa Benki ya Dunia na utekelezaji wake ni katika maeneo mapya 14, na mpaka sasa maeneo mapya matatu tayari yameshafikiwa ambayo ni Ngongo (Lindi Manispaa), Likunja (Wilaya ya Ruangwa) pamoja na Kagera.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe ameushukuru Uongozi wa Kata ya Likunja kwa kutoa Hekari 400 ambapo Kitivo cha Kilimo kitajengwa.
Aidha, Mhe Chikongwe ameendelea kwa kusema kuwa Mradi huu ni chachu ya maendeleo wilayani Ruangwa kwa sababu wananchi watajifunza namna ya kuongeza uzalishaji, idadi ya watu pia itaongezeka na hii itaenda kubadili sura ya Wilaya ya Ruangwa.
Pia, ametoa wito kwa wakazi wa Kata ya Likunja wajenge nyumba bora na za kisasa, kulima vizuri na kisasa zaidi ili kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Halmashauri kwa ujumla.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa