Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Hassan Ngoma ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uvunaji Wilaya, Amewataka wavunaji wa misitu kuwa waadilifu na kuvuna kiasi kinachoridhiwa na kamati ya uvunaji wa misitu.
Amesema "kumekuwa na tabia ya wavunaji kuomba idadi kubwa ya miti kisha kuvuna michache, hali hii inasababisha hoja za ukaguzi katika mapato kwani vijiji hukadiriwa makusanyo makubwa kutokana na uvunaji. kutovuna miti kwa idadi wanazoomba inaleta tofauti kubwa katika mapato halisi na yaliyotarajiwa.
Amesema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Uvunaji Wilaya kilichofanyika tarehe 12/08/2022 ikiwa ni kikao cha kwanza cha mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Ruangwa mjini.
Amewataka wavunaji wa misitu kufuata sheria na taratibu za uvunaji ili kutunza misitu hiyo na kuhakikisha inakuwa endelevu. Mhe. Mkuu wa Wilaya amekemea na kusisitiza wafanyabiashara wote kuacha kusafirisha mbao na magogo wakati wa usiku.
Aidha Mhe. Mkuu wa wilaya ametoa agizo kwa vijiji vyenye migogoro ya ardhi kuhakikisha migogoro hiyo inasuluhishwa kwa kukutana na kufanya mazungumzo ambayo yatapelekea makubaliano ya kuimaliza.
Akianisha migogoro hiyo Mhe. Mkuu wa Wilaya ametaja kijiji cha Namiegu na Nandeje, Mtondo na Nanjaru, Lichwachwa na Nahanga. Ameagiza kupewa taarifa ya hatua waliyofikia katika kutatua migogoro hiyo kabla ya tarehe 1/08/2022
"Naagiza wenye migogoro wakutane, wajadiliane na wasuluhishe kabla ya tarehe hiyo maana ikifika tarehe hiyo na bado mnaendeleza kuzozana nitatuma timu ya wataalamu waje wawaonyeshe mipaka ilipo kwa kufuata taratibu na sheria. Nafasi ya kupata suluhu kwa majadiliano mnayo, naomba muitumie"
Aidha alishukuru vijiji vilivyotoa mbao kwa ajili ya kujenga mabanda ya wafanyabiashara wadogo. Mabanda hayo yameboresha mazingira ya biashara kwa watu wetu pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya Halmashauri.
"Mmeonesha uzalendo na kuipenda Ruangwa yetu, mmerahisisha zoezi la upatikanaji mbao na mmerahisisha zoezi la ujenzi wa vibanda hivyo ambavyo vinatumika na wafanyabiashara wadogowadogo" amesema Ngoma.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa