Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrea Chikongwe amewataka washiriki wa mafunzo ya ufugaji kuku na samaki kutumia mafunzo hayo vizuri ili yawasaidie katika kujiendeleza kiuchumi.
Mhe. Chikongwe amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ufugaji kuku na samaki ambayo yameratibiwa na chuo cha Ufundi stadi (VETA) kanda ya Ruangwa ambayo yanaendelea katika kata ya Nandagala
Mheshimiwa Chikongwe alisema anategemea washiriki wote wa mafunzo hayo watatoka na vitu tofauti hivyo kwenda kuwasaidia watu wengine ambao hawajapata nafasi ya kushiriki.
"Nina imani mtatoka kivingine kabisa mtatoka hapa akili imebeba mambo mazuri tu kwani bahati mmeipata nyie zingatieni sana mnayofundishwa" amesema Mhe. Chikongwe.
Mhe. Chikongwe amebainisha kuwa wananchi wa Ruangwa wanapaswa kuitumia vema fursa hiyo ambayo maeneo mengine inapatikana kwa malipo na ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa na tija kwenye maisha yake.
"Pia Niwashukuru watu wa veta kuandaa mafunzo haya kwani ingewezekana mafunzo haya kupelekwa maeneo mengine ila yameletwa Nandagala na hakika wanaruangwa watanufaika na ujuzi huu" Amesema Mhe. Chikongwe.
Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Chuo hicho Mohammed Salim alisema kuwa wananchi wa Ruangwa wamepata bahati ya kupatiwa mafunzo hayo hivyo wanapaswa kuhakikisha wanayatumia kubadili mfumo wa ufanyaji wa shughuli zao.
Ndg, Salim ameongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajasiliamali wa Ruangwa na chuo chake kitahakikisha kinawafikia walengwa wote katika wilaya hiyo.
Vile vile alitoa Rai kwa wananchi wa Ruangwa kukimbilia fursa ya kusoma katika chuo cha VETA ambacho kinategemea kuanza mafunzo rasmi tarehe 01/06/2022 huku kikitarajiwa kutoa kozi tano ambazo ni ufundi ujenzi, ufundi selemala, ufundi magari, ufundi wa umeme majumbani na ushonaji na kozi hizo zote zitakuwa za muda mrefu na muda mfupi.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Bi. Asheri Nachinuku alishukuru uongozi wa chuo cha VETA Nandagala kwa kuona umuhimu wa kuwapatia mafunzo ya ufugaji kuku na samaki na kuahidi kuyatumia mafunzo hayo katika kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na VETA yanafanyika kwa muda wa siku 5 kuanzia Mei 17 hadi 21 mwaka huu.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa