Afisa anayesimamia Mradi wa uzalishaji mkaa kwa kutumia Teknolojia iliyoboreshwa Ndg. Othman Lugendo ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo ya uchomaji mkaa na upasuaji mbao kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kukata leseni za biashara ili kurasimisha shughuli zao.
Amesema, sasa ni wakati muafaka wa wafanyabiashara hao kutumia walichofundishwa na kuhakikisha shughuli zao zinatunza mazingira wakati zikiwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Amesema hayo leo tarehe 02/07/2022 wakati wa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wavunaji mkaa na mbao kwa kutumia teknolojia iliyoboreshwa yaliyofanyika ofisi ya kijiji cha Malolo.
"elimu mliyopata inapaswa kuanza kufanya kazi, natamani kuona nilichofundisha kipindi chote cha mafunzo haya kinawasaidia, natamani nikirudi nione mabadiliko ya mtu mmoja mmoja na kijiji kwa ujumla"
Faida zingine zinazotarajiwa kutokana na mradi ni kuongezeka kwa mapato ya kijiji ambayo itasaidia kukamilisha na kuanzisha miradi mbalimbali katika kijiji hicho.
Akihitimisha nasaha zake alisisitiza baada ya kukata leseni na kuwa kikundi rasmi wanaweza kuanza kuomba mikopo ya wanawake na Vijana inayotolewa na Halmashauri ili iweze kuwasaidia kuendeleza kazi zao.
Naye kaimu Afisa ardhi na maliasili ndugu Isihaka Panja aliushukuru uongozi wa Shirika la kuhifadhi misitu asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania ( MJUMITA) kwa kuwapelekea mafunzo hayo wananchi wa Malolo kama kijiji cha mfano.
Amesema Ndg Panja kazi wanazofanya washiriki hao zinahitaji sana mshikamano hivyo washikamane ili waweze kufanya kazi kwa uharaka na urahisi.
Aidha amesema wanachama wa vikundi hivyo wanapaswa kuanza kufanya kazi sasa kwani mabadiliko yanaanza sasa na si baadae.
"mnapaswa kuanza uchomaji na uvunaji mbao kwa kufuata taratibu mlizoelekezwa".
Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo waliopata washiriki kwa vitendo yanayoratibiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa