Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kutenga asilimia kumi ya kila mapato yake kabla ya matumizi kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana.
Aliyasema hayo wakati wa kikao cha baraza maalum la waheshimiwa madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Halmashauri ya Ruangwa zilizojitokeza wakati wa ukaguzi uliofanywa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa fedha za Serikali kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Rutesco Ruangwa mjini.
“Siyo kwamba hampati hizo fedha mnazipata ila amzipi kipaumbele asilimia10 mnazotakiwa mpeleke kwenye mfuko wa vijana na wanawake mkipata hela hata kama milioni 100 tengeni hela ya kurudisha kwenye mfuko wa vijana na wanawake kabla amjaanza matumizi mengine" amesema Mkuu wa Mkoa.
"Hili jambo la kutopeleka fedha kwenye huu mfuko linataka kuonekana kama ni suala la kawaida sasa bajeti ya mwakani ikija na mapungufu ya kupeleka asilimia 10 katika mfuko wa vijana na wanawake sitoipokea na kuipeleka kwenye kamati ya bunge" alitilia mkazo Mkuu wa Mkoa.
Aidha aliwataka waheshimiwa madiwani kusimamia na kuhakikisha fedha hizi zinapatikana na kuwafikia walengwa ambao ni wanawake na vijana ili waweze kujiajiri na kujiongezea kipato chao.
"Hao wanaotakiwa kurudishiwa hizo fedha ni wapiga kura wenu sasa msipowasimamia wakapata wanachostahili kupata mnakuwa amuwatendei haki simamieni hili suala liishe kwani ndiyo linaloleta hoja nyingi kila mwaka" amesema Zambi.
Hata hivyo alimtaka Mkurugenzi kuwa makini na vikundi vinavyoomba hiyo mikopo kwasababu kuna vikundi ambavyo havitambuliki na kukosa mpango mkakati endelevu wa mradi wao na kuona kama una faida sababu fedha hizo zitatakiwa kurejeshwa.
“ Mkurugenzi unapaswa kufuatilia fedha unazopeleka kwenye vikundi zinatumikaje ni wajibu wako kupeleka fedha na kuzifuatilia zifuatilie na zisimamie kwa kushirikiana na wataalam wengine wasaidieni vikundi hadi zitoe faida.”Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Zambi.
Hata hivyo aliwapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kupata hati safi katika ukaguzi huo na kuwataka watendaji kuendelea kutimiza majukumu yao ya kila siku ili kupunguza hoja ambazo nyingi siyo nzito na uwezo wa kufanya hivyo sababu halmashauri hiyo ina viongozi na watendaji wachapakazi.
Baraza maalum la kupitia hoja za ukaguzi wa hesabu kwa mwaka 2016/2017 lilifanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa, wageni kutoka ofisi Ras ,Waheshimiwa madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa