Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia tawi lake la Mikocheni, kimeonesha kuridhishwa na maendeleo ya kilimo cha minazi wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, baada ya kufanya ziara leo Aprili 15, 2025. ya kukagua mashamba ya minazi iliyoanzishwa kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Ziara hiyo ni sehemu ya ufuatiliaji wa kitaalamu wa utekelezaji wa mpango wa kuendeleza zao la mnazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, ambapo miche ya minazi ilisambazwa kwa wakulima ili kuinua kipato chao na kuimarisha uchumi wa maeneo ya pwani kwa ujumla.
Naye, Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano kutoka TARI Mikocheni, Bi. Vidah Yosia Mahava, ambaye ameongoza ziara hiyo, amesema kuwa wakulima wameonesha juhudi kubwa katika kutunza miche hiyo na wameitikia vyema teknolojia waliyopewa.
“Tunaona maendeleo mazuri sana ya minazi hii, wakulima wameonesha moyo wa kujituma na wameitikia vyema teknolojia na elimu waliyopewa. Hili ni jambo la kufurahisha na linatupa matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa zao hili,” amesema Bi. Mahava.
Katika ziara hiyo, wataalamu wa TARI wametembelea mashamba ya wakulima na kushuhudia hali ya miche, huku wakitoa pongezi kwa juhudi zinazofanywa na wananchi katika kuitunza. Wamewasihi wakulima kuendelea kufuata mbinu bora za kilimo ili kuhakikisha miche hiyo inakua kwa mafanikio na kuleta matokeo chanya.
Aidha, Bi. Mahava amesisitiza kuwa TARI itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu na kufuatilia maendeleo ya minazi hiyo ili kuhakikisha mpango huo unaleta tija kwa wakulima.
Ikumbukwe, Zao la mnazi linaelezwa kuwa na faida mbalimbali zikiwemo uzalishaji wa nazi, mafuta, mbao na bidhaa nyingine, hivyo kuwekeza katika zao hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendeleza kilimo chenye tija.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa