Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambae pia ni mlezi wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Lindi, Mhe. Zuberi Ali Maulid, ameahidi kufikisha salamu za uhitaji wa vifaa tiba katika jengo la wodi ya wanaume na wanawake lililojengwa katika kituo cha Afya kata ya Nandagala wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kufanya ziara ya kutembelea katika kituo hicho mapema Februari 6 Mwaka huu na kukagua mradi wa ujenzi wa wodi hizo zilizokamilika ambapo zinatajwa kutoanza kutumika kutokana na ukosefu wa vifaa tiba.
Mhe. Zuberi amepongeza juhudi kubwa ya serikali iliyofanywa katika kuboresha miundombinu na kubainisha kuwa hayo ni kwa mujibu wa ilani na kuwaeleza wananchi kwamba waendelee kuimani serikali iliyo madarakani na chama chake kwakua wanatekeleza waliyoahidi katika kuwapatia wananchi maendeleo.
“Naamini hata ninyi mnaona kasi ya maendeleo na uboreshaji wa miundombinu inayotokana na Imani mlioipa serikali inayoongozwa na chama cha mapinduzi, muendelee na moyo huo nasisi tutaendelea kuhakikisha ilani inatekelezwa ili kutimiza adhma ya kuwapatia maendeleo wananchi” alisema Mhe. Zuberi
Awali mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Ruangwa Ndg,Ibrahim Ndolo, alipokua anatoa salamu za pongezi kwa uongozi wa chama hicho Taifa alieleza Pamoja na mambo mazuri yanayotekelezwa na ilani lakini ameomba kusaidiwa vifaa tiba kwa ajili ya kuifanya wodi hiyo mpya iliyojengwa iweze kutumika.
“umeona mafedha yameletwa hapa matumaini yetu wana ruangwa majengo haya yatumike, tumekosa vifaa tiba, sasa hili ndilo ninalokukabidhi mimi tena nina kupigia magoti hapa, fanya uwezavyo utusaidie vifaa tiba ili majengo haya yaweze kutumika” alisema ndolo huku akiwa amepiga magoti mbele ya Mhe. Zuberi ambae ni spika wa baraza la wawakilishi Zanzibar.
Katika hatua nyingine Mhe. Zuberi ametembelea shule ya sekondari ya wasichana Ruangwa ambayo imefunguliwa hivi punde na kusifu miundombinu iliyojengwa shuleni hapo huku akiwasiki wanafunzi walioanza kusoma katika shule hiyo kuwa na bidii.
Mhe. Zuberi yupo katika ziara ya kikazi mkoani Lindi akiwa kama Mlezi wa chama cha Mapinduzi ambapo amekua akipita katika wilaya za mkoa wa Lindi kukagua miradi ya maendeleo kuona namna ilani ya chama kilichopo madarakani inavyotekelezwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa