Serikali kupitia Tume ya Mpango na matumizi bora ya Ardhi sambamba na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imemaliza migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji leo Machi 13, 2024 walivyofanya ziara ya ukaguzi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji cha Namkatila Kata ya Matambalale Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timotheo Mzava amewataka wananchi kusimamia mipango na sheria ndogondogo zilizoundwa kijijini hapo ili kuleta tija na kuepusha migogoro ya ardhi hivyo wanakijiji hao wameunda sheria ndogondogo kama vile, Kijiji cha Namkatila ni kwa ajili ya wakulima tu na sio wafugaji na Mita 60 kutoka kwenye Mto Mbwemkuru mwananchi yeyote haruhusiwi kumiliki ili kila mmoja aweze kunufaika na eneo hilo.
Ziara hiyo pia imehusisha kugawa hati miliki za kimila 734, hati miliki ya Ardhi ya kijiji, daftari la ardhi ya kijiji, pamoja na ripoti ya mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Ndugu Geophrey Mizengo Pinda amewataka wakulima kutumia hekima kutatua migogoro ya ardhi katika jamii na baraza la ardhi la Kata litumike kutoa elimu kwa jamii kuhusu ardhi.
"Na katika ugawaji wa ardhi kusifanyike janja janja yeyote kila mmoja apate haki yake kwa kupata sehemu yake ya ardhi anayostahili na ikumbukwe kuwa Watendaji hawaruhusiwi kuuza ardhi pasi na makubaliano ya kijiji na kwa upande wa Wilaya lazima ihusike katika utoaji wa kibali cha mwisho kwa ajili ya wawekezaji" Amesema Pinda
Aidha amewasisitiza wananchi kutunza hati miliki zao za kimila na si kuazimishana ambapo hati hizo zimetambuliwa katika makundi ya Makazi na Mashamba na ndio ulinzi tosha wa Ardhi ya mwananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Hassan Ngoma amewashukuru wananchi kwa kushiriki katika mchakato wa kupima na kupanga kwa pamoja matumizi ya Ardhi ya kijiji cha Namkatila.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa