Shirika la Sports Development Aid (SDA), kwa kushirikiana na Liike—shirika la kimataifa lenye makao yake makuu nchini Finland limeendesha mafunzo ya huduma ya kwanza kwa walimu na wanafunzi kutoka shule za sekondari 16 zilizopo katika Wilaya ya Ruangwa, leo Aprili 29, 2025
Mafunzo hayo yamefanyika katika Shule ya Sekondari Kassim Majaliwa yakilenga kuongeza maarifa na ujuzi wa msingi juu ya huduma ya kwanza kwa ajili ya kusaidia katika mazingira ya michezo, masomo na afya kwa ujumla, yakihusisha vipindi vya nadharia na vitendo, ambapo washiriki wamefundishwa namna ya kushughulikia hali za dharura kama vile kupoteza fahamu, majeraha ya viungo, kupumua kwa shida na ajali nyingine zinazoweza kutokea wakati wa shughuli za kila siku shuleni, hasa michezoni.
Aidha, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka SDA, Ndugu Ramson Lucas, amesema kuwa ushirikiano kati ya SDA na Liike ni sehemu ya mkakati mpana wa kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania katika nyanja mbalimbali za kijamii, kielimu na kiafya.
“kuwa kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa walimu na wanafunzi ni hatua ya msingi ya kuhakikisha shule zinakuwa maeneo salama na yenye ulinzi wa afya kwa washiriki wote.” Amesema Lucas.
Vilevile, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopata, wakisema kwamba kabla ya hapo walikosa uelewa wa kutosha kuhusu hatua sahihi za kuchukua wakati wa matukio ya dharura. Wamesema kuwa sasa wamejiamini zaidi kushughulikia hali kama kuzimia kwa mwanafunzi, kujeruhiwa au kupata mshtuko wa kiafya wakati wa michezo au vipindi vya masomo.
Kwa ujumla, mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za mashirika ya kimataifa na wadau wa elimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Kwa kutoa elimu ya huduma ya kwanza, SDA na Liike wamechochea utamaduni wa kuzingatia usalama na afya shuleni, na hivyo kuongeza ufanisi katika maendeleo ya elimu na ustawi wa jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa