Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa limeendelea kuvutia wakulima na wadau wa kilimo katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane Kanda ya Kusini, yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Ngongo, kupitia utoaji wa elimu ya kilimo cha kisasa cha alizeti chenye tija kubwa kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Afisa Ugani wa Wilaya ya Ruangwa, Frank Sinyangwe, mbegu ya alizeti inayofundishwa kwa wakulima katika banda hilo ni aina ya mbegu bora kutoka kampuni ya Seedco, ambayo hukomaa haraka kati ya siku 75 hadi 90 na huweza kustawi vizuri katika maeneo ya joto kali au baridi.
“Gunia moja la alizeti la kilo 75 linaweza kutoa hadi lita 30 za mafuta, na kwa ekari moja mkulima anaweza kuvuna kati ya magunia 15 hadi 20 ikiwa atalima kwa kufuata kanuni sahihi za kilimo, hivyo nawasihii wakulima kuichangamkia mbegu hii kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla,” amesema Sinyangwe
Aidha, mbegu hiyo imepewa sifa ya kuwa “mbegu mkombozi”, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mavuno mengi kwa muda mfupi, na hivyo kuwa chachu ya kuongeza kipato kwa wakulima, kulingana na maelezo yaliyotolewa katika banda hilo.
Vilevile, wakulima mbalimbali waliotembelea banda hilo wameeleza kuvutiwa na teknolojia na maarifa yanayotolewa, wakisisitiza kuwa sasa wamefunguka macho kuhusu fursa zilizopo kwenye kilimo cha mazao ya mafuta.
Kwa ujumla, banda hilo limeendelea kuwa moja ya vivutio vikubwa katika maonesho hayo, likihamasisha wakulima kuwekeza kwenye kilimo bora cha alizeti ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa kaya na taifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa