Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nandagala wilayani Ruangwa wanatarajiwa kuanza kupata lishe bora kupitia mpango wa lishe shuleni baada ya kukabidhiwa kuku 1,000 aina ya Hyline Brown, kupitia Mradi wa School Feeding Eggs Program unaotekelezwa na Kituo cha Utafiti wa Mifugo Tanzania Kanda ya Kusini (TARLI), kwa ufadhili wa Ofisi ya Sapling IRLI.
Akizungumza leo Julai 5, 2025 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TARLI, Mkurugenzi wa Utafiti Dkt. Andrew Chota, amesema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha afya za watoto kwa kuwapatia protini ya kutosha, kuwajengea stadi za maisha, pamoja na kuongeza kipato kwa shule.
“Kuanzia wiki ya 24 ya kuku hawa, kila mwanafunzi katika Shule ya Msingi Nandagala ataanza kupata yai moja kwa siku. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora na uwezo mzuri wa kujifunza,” amesema Dkt. Chota.
Aidha, Dkt. Chota ameeleza kuwa wataalamu wa TARLI wataendelea kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo kwa kuhakikisha usafi wa banda, utoaji wa chanjo kwa wakati na maendeleo ya afya ya kuku hao ili kuwaepusha na magonjwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndg. Zuberi Sarahani, mara baada ya kupokea rasmi kuku hao kwa niaba ya Halmashauri, ametoa shukrani zake za dhati kwa wafadhili hao, akisisitiza kuwa Serikali ya Kata pamoja na Uongozi wa Shule wanapaswa kusimamia mradi huo kwa makini ili kuleta tija iliyokusudiwa.
“Mradi huu si tu wa kutoa mayai, bali unajenga kizazi cha vijana wenye afya bora, wanaojifunza kwa vitendo stadi za maisha, na kuisaidia shule kujitegemea,” alisema Ndugu Sarahani.
Wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nandagala wamepokea mradi huo kwa shangwe na matumaini makubwa, wakisema kuwa utasaidia kupunguza utapiamlo kwa watoto na kuongeza ari ya mahudhurio darasani.
Mradi wa School Feeding Eggs Program ni mfano wa ubunifu unaoonyesha namna tafiti za kisayansi na ushirikiano wa taasisi za Serikali na binafsi zinavyoweza kutatua changamoto za msingi katika elimu na afya za watoto mashuleni.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa