- Serikali kuchangia gharama za chanjo ili kuwapunguzia wafugaji mzigo wa matibabu
- Zaidi ya dozi 12,000 za chanjo zitatumika kudhibiti ugonjwa wa mapafu na Sotoka kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo
- Hereni za utambuzi wa mifugo kugawiwa bure kwa ajili ya usimamizi bora wa afya ya mifugo
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mwl. George Mbesigwe, amepokea jumla ya dozi 12,500 za chanjo za mifugo leo tarehe 27 Juni 2025, kwa ajili ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo.
Katika chanjo hizo, dozi 3,000 zimetengwa kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe (CBPP), huku dozi 9,500 zikiwa ni kwa ajili ya ugonjwa wa Sotoka (PPR) kwa mbuzi na kondoo.
Akizungumza wakati wa upokeaji wa Chanjo hizo Mwl. Mbesigwe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa msaada mkubwa kwa sekta ya mifugo na kwa kutambua mchango wa wafugaji katika uchumi wa taifa.
“Natoa pongezi na shukrani kwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya mifugo, kupitia chanjo hizi, wafugaji wetu watanufaika kwa kiwango kikubwa kwa kuwa na mifugo yenye afya na tija zaidi,” amesema Mbesigwe.
Aidha, kampeni hiyo inalenga kuhakikisha mifugo inalindwa dhidi ya magonjwa hatari kwa gharama nafuu, ambapo ng’ombe watachanjwa kwa ruzuku ya Serikali; badala ya shilingi 1,000, wafugaji watalipa shilingi 500 tu, na Serikali kuchangia shilingi 500.
Vilevile, kwa mbuzi na kondoo, chanjo itatolewa kwa shilingi 300 badala ya 600, ambapo Serikali itachangia nusu ya gharama hiyo ili kupunguza mzigo kwa wafugaji.
Zaidi ya hapo, hereni za utambuzi kwa mifugo zitagawiwa bure kwa wafugaji wote watakaoshiriki kampeni hiyo.
Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kitaifa ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 16 Juni 2025, mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha afya ya mifugo na kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa