Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imeshika nafasi ya kwanza kwa matumizi bora ya Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST) kwa Kanda ya Kusini, hatua inayoonesha dhamira ya halmashauri hiyo katika kuimarisha uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma.
Akizungumza leo Aprili 14, 2025, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo huo, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Nkowe, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mwl. George Mbesigwe, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo.
“Tumefanikiwa kushika nafasi ya kwanza Kanda ya Kusini na ya nne kitaifa katika matumizi ya mfumo wa NeST, jambo linalothibitisha juhudi zetu katika kusimamia ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu,” amesema Mwl. Mbesigwe.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Watendaji wa Taasisi za Umma ili kuhakikisha mfumo huo unatumika kikamilifu katika kuhakikisha ununuzi wa umma unakuwa wenye tija na uwazi.
Mafunzo hayo yamehusisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ruangwa, yakiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha utekelezaji wa mfumo wa NeST unafanyika kwa ufanisi nchini kote.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa