Wilaya ya Ruangwa leo tarehe 6 Desemba 2024, imefanya kongamano maalum kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, likihudhuriwa na makundi mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wanafunzi, viongozi wa dini, kamati ya siasa ya Wilaya, na wawakilishi wa kundi la wenye ulemavu.
Mgeni rasmi wa kongamano hilo alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Andrew Chikongwe, ambaye ametumia fursa hiyo kupongeza mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana tangu uhuru. “Tumepiga hatua kubwa sana tangu uhuru mpaka leo,” amesema Chikongwe, akiweka msisitizo kwenye maendeleo yaliyoshuhudiwa ndani ya Wilaya ya Ruangwa na taifa kwa ujumla.
Aidha, mtoa mada katika sekta ya uchumi, Ndugu Rashidi Hassan Nakumbya, ameangazia maendeleo ya miundombinu na ustawi wa uchumi, akisema, “Tumepiga hatua kubwa sana katika Wilaya yetu. Tuna barabara nzuri, vijiji vyote vinafikika, na bei nzuri za mazao ni miongoni mwa mafanikio makubwa.”
Katika sekta ya afya, Bi Hawa Mpinga amebainisha mabadiliko makubwa tangu kipindi cha uhuru, akisema, “Kabla ya uhuru, akina mama walikuwa wanapoteza maisha kwa ukosefu wa huduma bora za afya. Leo tunajivunia hospitali kubwa na vituo vya afya vya kutosha. Magonjwa kama ukoma, ndui, na pepopunda ni hadithi sasa.”
Kwa upande wa ukatili wa kijinsia, Bi Lucia Chitanda ameeleza jinsi miaka 63 ya uhuru imeimarisha uhuru wa kijinsia, akisema, “Zamani wakoloni walitunyima fursa, lakini sasa ukatili unakemewa, taarifa zinatolewa kwa wakati, na wahusika wanachukuliwa hatua.”
Naye, Mama Magehema ameeleza mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, akionesha tofauti kubwa iliyokuwepo kabla ya uhuru, baada ya uhuru, na hali ya sasa. Amepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira bora ya kujifunzia ambayo yameongeza viwango vya ufaulu nchini
“Zamani, shule zilikuwa hazifaulishi kabisa. Ilikuwa kawaida kuona mtu mmoja au wawili tu wakifaulu, na ukikuta watatu ni bahati kubwa sana. Lakini siku hizi, ufaulu umeongezeka sana karibu darasa zima linafaulu. Kuna walimu wa kutosha, watoto wanafanya vizuri, na miundombinu imeboreshwa na ni rafiki sana kwa kujifunzia. Kwa kweli, tumepiga hatua kubwa,” amesema Mama Magehema.
Kongamano hilo limeonesha uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Ruangwa, huku likiwa na lengo la kutafakari mafanikio yaliyopatikana na kuhamasisha juhudi zaidi za maendeleo kwa miaka ijayo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa