Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wameadhimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya bonanza la michezo mbalimbali leo Aprili 26, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Dodoma, Kata ya Nachingwea.
Katika bonanza hilo, washiriki wamehamasika kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mbio za pole (jogging), mchezo wa kutembea ndani ya magunia, kuvuta kamba, rede pamoja na mpira wa miguu, kwa lengo la kuimarisha afya, mshikamano na kuendeleza umoja wa kitaifa.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo yamewaleta pamoja wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ruangwa, wakionesha mshikamano mkubwa na furaha ya kuendeleza Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, wananchi wameshiriki michezo kwa ari na morali ya hali ya juu huku wakihimizwa kuendeleza mshikamano katika maisha yao ya kila siku bila kusahau kuuenzi Muungano.
Sambamba na hilo, viongozi wa Wilaya wametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Hatimaye, bonanza hilo limehitimishwa kwa ujumbe wa kuwaasa wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano kama tunu muhimu za taifa.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu inasema:
“Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa, Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.”
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa