Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Ruangwa imefanya zoezi la usafi likijumuisha viongozi, watumishi wa umma, na wananchi, zoezi hilo limefanyika leo Desemba 5, 2024, katika maeneo ya Stendi ya Mabasi na Soko Kuu la Ruangwa, likilenga kuboresha mazingira na afya ya jamii.
Zoezi hilo muhimu limeongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Zuhura Rashid, ambaye ameisisitiza umuhimu wa wananchi na wafanyabiashara kuanzisha utaratibu endelevu wa usafi
Aidha, Mhandisi Zuhura Rashid, amesisitiza kwamba mazingira safi uchochea maendeleo ya wananchi maana wanaweza kufanya kazi zao za kila siku kwa amani na utulivu bila kusumbuliwa na magonjwa ama mafuriko wakati wa mvua.
“Hali safi ya mazingira inalinda afya na kuimarisha maendeleo yetu, tujitahidi kuuweka mji wetu safi hasa tunapoelekea msimu wa mvua ili kuepuka magonjwa hatarishi kama kipindupindu,” amesema Mhandisi Zuhura.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ruangwa, Ibrahim Ndoro, amesisitiza umuhimu wa kila mfanyabiashara kuwajibika katika usafi.
“Lazima tuhakikishe kila mmoja anafuata sheria za usafi. Tushirikiane kuweka Wilaya yetu kuwa kielelezo bora cha maendeleo,” amesema Ndoro huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokiuka.
Naye, Diwani wa Kata ya Ruangwa, Mhe. Alipa Mponda, amewapongeza washiriki wa zoezi hilo kwa uzalendo wao.
“Kuacha shughuli zako binafsi na kushiriki zoezi hili ni ishara ya upendo kwa nchi yako. Tuendelee na moyo huu hata baada ya maadhimisho haya,” amesema.
Maadhimisho ya kilele cha Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara wilayani Ruangwa yatafanyika Disemba 8, 2024, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Likangara kuanzia saa 4:00 asubuhi. Shughuli hizo zitaongozwa na kaulimbiu mpya ya mwaka huu:
“JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU.”
Ikumbukwe, shughuli mbalimbali zikiwemo midahalo, kongamano la maendeleo, michezo, na uandishi wa insha zitafanyika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, yakiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuhamasisha uzalendo kwa maendeleo endelevu.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa