Katika kuhakikisha utekelezaji wa afua za lishe unazingatia malengo ya kitaifa na kimkakati, Wilaya ya Ruangwa imefanya kikao cha tathmini ya robo ya tatu ya mkataba wa lishe, kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Hassan Ngoma, kilichofanyika leo Mei 2, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Kikao hicho kimekusudia kutathmini utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza, pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha jamii inanufaika na huduma bora za lishe, lakini pia kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya lishe wakiwemo maafisa wa afya, elimu, kilimo, mashirika yasiyo ya kiserikali na viongozi wa kijamii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Hassan Ngoma alisema amempongeza mratibu wa Lishe wa Wilaya kwa kazi nzuri anayoifanya.
“Nimpongeze Mratibu wa Lishe wa Wilaya kwa kazi kubwa anayofanya kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele, mafanikio tuliyoyapata hadi sasa ni matokeo ya jitihada za pamoja za wataalamu na wadau wote wa maendeleo.” Amesema Mhe. Ngoma.
Aidha, Mratibu wa Lishe wa Wilaya ndugu Barikieli Gulmay Duwe ametoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe ikiwemo utoaji wa elimu ya lishe mashuleni, usambazaji wa virutubisho, na kampeni za uhamasishaji wa lishe bora kwa wazazi na walezi. Alibainisha kuwa pamoja na changamoto za rasilimali na mwitikio wa baadhi ya jamii, hatua kubwa zimepigwa katika kupunguza kiwango cha utapiamlo.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho wametoa mapendekezo ya kuimarisha usimamizi, kuongeza bajeti ya lishe katika ngazi ya Halmashauri, na kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa lishe bora. Kikao kimehitimishwa kwa kuazimia kila sekta kuendelea kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kufanya ufuatiliaji wa karibu zaidi kwa kipindi kijacho.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa