Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, ameongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 leo Septemba 08, 2025, kikilenga kujadili mafanikio, changamoto na kuweka mikakati mipya ya lishe.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kimehusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama, wakuu wa idara na vitengo, watendaji wa kata, maafisa lishe wa kata zote pamoja na maafisa wa afya. Lengo kuu kimekuwa kutathmini utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha miezi mitatu, kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha jamii inanufaika na huduma bora za lishe.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ngoma amewapongeza watendaji wa kata zilizofanikisha viashiria vya lishe kwa kufikia malengo, amewataka waendelee kufanya kazi kwa bidii.
“Hongereni sana kwa kazi nzuri, mnajituma sana, nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwakumbusha kwamba kila kitu kinawezekana, fanyeni kazi kwa bidii na kwa kujituma, nategemea mwaka huu kata zote 22 zitafikia malengo kwa asilimia 100,” amesema Mhe. Ngoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amewataka watumishi wanaosimamia masuala ya lishe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha Ruangwa inakuwa ya kwanza kitaifa.
“Fanyeni kazi bila visingizio, tunao uwezo wa kufikia malengo kwa kila kata maana Serikali imeweka mazingira wezeshi, nategemea kuona tunavuka malengo kwa robo ya kwanza ya mwaka huu, kwa sasa tunaongaza kimkoa nataka tuongoze kitaifa” amesema Chonya.
Aidha, Mratibu wa Lishe wa Wilaya, Ndugu Barikieli Gulmay Duwe, ameeleza kuwa utekelezaji wa afua za lishe umejikita kwenye elimu mashuleni, usambazaji wa virutubisho na kampeni za uhamasishaji.
Washiriki wa kikao wamependekeza kuongeza kuwa juhudi ziongezwe kwa usimamizi wa karibu, ili kuimarisha utekelezaji na uboreshaji wa Lishe. Lakini pia, wameomba zoezi la kutoa elimu kwa wananchi liwe endelevu ili kuwajengea uelewa mkubwa zaidi.
Kikao kimehitimishwa kwa makubaliano ya kila sekta kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuimarisha ufuatiliaji katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku wadau wakiahidi kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuhakikisha malengo ya kitaifa ya lishe yanafikiwa kwa ufanisi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa