Kikao cha Maabara ya Elimu ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kimefanyika leo, Desemba 2, 2024, katika bwalo la Shule ya Sekondari Ruangwa, kikilenga kuchambua changamoto, mafanikio, na mbinu bora za kuboresha sekta ya elimu.
Kikao hicho, ambacho kimeongozwa na Afisa Elimu Msingi wa Wilaya, Mwalimu George Mbesigwe, kimewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Maafisa Elimu, wawakilishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu, walimu wakuu, wakuu wa shule, na maafisa kutoka Idara ya Elimu, ajenda kuu zimehusu tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya mwaka 2024, pamoja na mipango ya kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu wilayani.
Aidha, mada zilizojadiliwa ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao cha maabara kwa mwaka huu, tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati, changamoto zinazokabili sekta ya elimu, mafanikio yaliyopatikana, na suluhisho za changamoto hizo, Zaidi ya hayo, kikao hicho kimeweka mkazo katika mafunzo endelevu kwa walimu ili kuwajengea uwezo zaidi wa kufanikisha malengo ya kielimu.
Vilevile, sehemu ya majadiliano imejikita pia katika utekelezaji wa shughuli za michezo, hususan mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA, ambayo yanatajwa kuchangia maendeleo ya wanafunzi kiakili, kimwili, na kijamii. Isitoshe, washiriki wamesisitiza umuhimu wa michezo shuleni kama sehemu ya kukuza vipaji na kuimarisha afya ya wanafunzi.
Hata hivyo, changamoto kama upungufu wa walimu na miundombinu duni bado ni vikwazo vilivyojadiliwa kwa kina. Akizungumza katika kikao hicho, Mwalimu George Mbesigwe amesema juhudi za pamoja kati ya walimu, wazazi, na Serikali zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua viwango vya elimu wilayani Ruangwa.
“Lazima tuendelee kushirikiana kama jamii ili kuhakikisha tunapunguza changamoto na kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wetu,” amesema Mbesigwe.
Kwa upande mwingine, wadau wa elimu wamekubaliana kuwa mpango mkakati wa elimu unapaswa kuzingatia vipaumbele vinavyolenga kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza vifaa vya kujifunzia, na kushughulikia upungufu wa walimu. Kadhalika, wamesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya shule na jamii ili kufanikisha malengo hayo.
Ikumbukwe, kikao hicho kinaonekana kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inapata msukumo mpya na kufanikisha maendeleo endelevu wilayani Ruangwa, washiriki wameonyesha matumaini kuwa utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho utaleta matokeo chanya.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa